Header Ads

MKURUGENZI MANISPAA YA MOROGORO ATOA WITO KWA JAMII NA WAZAZI KUONDOKANA NA MILA KANDAMIZI DHIDI YA WATOTO WAKIKE.


Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, akisalimiana na Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Msamvu ''B'' ikiwa ni furaha kuashiria Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa kike. 

MKURUGENZI wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, ametoa wito kwa Jamii na Wazazi kuachana na mila na desturi zinazolenga kumkandamiza Mtoto wa kike.

Kauli hiyo ameitoa leo, Oktoba 12, 2020 ,  ikiwa imepita siku moja tangia Mtoto wa kike aadhimishe sikukuu hiyo ambapo hufanyika kila mwaka ifikapo  Oktoba 11,2020.

Akizungumza na Waandishi wa habari, Lukuba,  ameitaka  Jamii na Wazazi kuacha mila na desturi ya kuwalazimisha watoto wa kike kuolewa wakiwa na umri mdogo na badala yake wapeleke watoto shule wakapate elimu ili waweze kutimiza ndoto zao.

“Inashangaza sana kuona bado mnazikumbatia mila na desturi kandamizi zinazo wanyanyasa Wanawake,kwani Wanawake pia wanayo nafasi na haki ya kupanga na kuamua mambo hivyo tuache kuwaamulia vitu wasivyovitaka, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, imekuwa mstari wa mbele kuwaamini Wanawake  hususani katika nyadhifa mbalimbali za kiutawala na Uongozi, hivyo lazima tuwape vipaumbele Watoto wa kike na kuwaondolea mila kandamizi ili wafikie malengo katika Ujenzi wa Taifa ”Amesema Lukuba.


Lukuba, amesema bado kuna kesi ambazo zinatokea za Watoto wa kike kulazimishwa kuingi katika mahusiano , hivyo katika hilo  Manispaa yake hawatawafumbia macho watu wa namna hiyo, atahakikisha kwa kushirikiana na  vyombo vya dola ili watu wanaoenda kinyume na haya wakamatwe na kuchukuliwa  hatua kali kwani kitendo hicho kinatambulika kama ubakaji kwani vitendo hivyo wamekuwa wakifanyiwa mabinti wenye umri mdogo sana.

“Nasema hivi hatuwezi kuwafumbia macho watua ambao bado wanaendeleza mila na tamaduni ambazo hazina faida yeyote kwa jamii sio wa kuwachekea chekea nataka wote wakamatwe na kesi zao ziende mahakamani haraka ili tabia hii iweze kukoma na iwe fundisho, tunataka Jamii zenye uelewa dhidi ya Mtoto wa kike, kwahiyo tutahakikisha tunashirikiana vizuri na Wazazi ili haya yanayofanyika yasitokee, Ustawi wa Jamii upo naamini wanafanya kazi zao vizuri sana katika haya ya unyanyasaji, tukiona mtu hawezi kubadilika basi vipo vyombo ambavyo vitambadilisha kwa mujibu wa Sheria za nchi" Ameongeza Lukuba.


Aidha, amewataka Wazazi na jamii kuwekeza elimu kwa Watoto wao wa  kike badala ya kuwa na imani za tofauti za kuwasomesha Watoto wa kiume pekee.

Pia ,amewataka Wazazi kukaa na Watoto wao kuwafundisha maadili mazuri na tabia njema kwani maadili mengi yanapotea kutokana na Wazazi wengi kusahau majukumu yao katika maadili ya Watoto wao.


Mwisho,  amewaonya watu wenye mila potofu katika Manispaa ya Morogoro ,  na kusisitiza kuwa hilo halikubaliki kisheria na yeyote atakaebainika anaendelea na zoezi hilo hatosita kumchukulia hatua dhidi yake hivyo wanapaswa kufuata sheria na taratibu kwa kutenda haki kwa watoto wa kike.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.