Header Ads

MKURUGENZI MANISPAA YA MOROGORO AWAASA WANANCHI KUTUNZA VYAKULA.


        Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba.

MKURUGENZI wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba,  amewataka wakazi wa Manispaa ya Morogoro  kuhifadhi chakula ili kiweze kuwasaidia kwa siku zijazo.

Kauli hiyo ameitoa leo Oktoba 16,2020 ikiwa ni siku  ya Chakula duniani.

Akizungumza juu ya suala hilo, amesema kuwa lazima wananchi wajifunze jinsi ya kutunza vyakula na kuweka akiba ili kuepuka suala la njaa.

“ Ni  wajibu kwa wananchi wote wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro,  kutunza chakula ili kiweze kuwasaidia kwa siku zijazo, tusiuzee vyakula vyetu , watoto wanahitaji lishe bora sasa tukielekeza kuuza vyakula vyote bila kuwa na akiba  njaa zitatukuta na tutaishi maisha ya kutangatanga"Amesema Lukuba.

Aidha, Lukuba, amewataka Wazazi wajenge tabia za kuwapatia watoto lishe bora ili waweze kujengeka kiakili na kuongeza viwango vya ufaulu darasani.

Mbali na hayo, amewataka Wazazi kutoa pesa za michango ya vyakula Shuleni ili watoto waweze kusoma vizuri wakiwa wameshiba.

"Huwezi ukapata matokeo mazuri ya mtoto wako wakati unashindwa kumpatia chakula , mtoto anashinda shule masaa 9 sasa kama hajapata chakula unafikiri atakuwa na uwezo mzuri wa kufikiri? niwaombe Wazazi watoe michango ya  vyakula ili watoto wao waweze kusoma vizuri darasani "Ameongeza Lukuba.

Hata hivyo, amezikumbusha jamii zijenge utaratibu wa kuwapatia Watoto wadogo kunywa maziwa ili wajengeke kiakili, kwani maziwa yanasaidia sana mtoto kuwa na akili nzuri na uwezo mkubwa wa kufikiria. 



No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.