Header Ads

MANISPAA YA MOROGORO YAADHIMISHA SIKU YA UKIMWI DUNIANI

 



KILA  ifikapo Desemba Mosi,Dunia huadhimisha siku ya UKIMWI, lengo likiwa ni kuikumbusha Jamii kuhusu ugonjwa huu, kutafakari hatua zilizopigwa katika kukabiliana nao, kukumbuka na kuenzi mamilioni ya watu waliopoteza maisha kutokana na ugonjwa huu, lakini pia kutoa elimu na kuweka mikakati ya pamoja katika kudhibiti na kutokomeza VVU/UKIMWI.

Kuelekea kilele cha maadhimisho hayo leo Desemba 01, 2024 ,Manispaa ya Morogoro   imeadhimisha siku ya UKIMWI Duniani ,maadhimisho hayo yamefanyika  Zahanati ya Malipula  Kata ya Chamwino  na kuhudhuriwa na Viongozi, Taasisi pamoja na Asasi mbalimbali

Akizungumza wakati wa hotuba yake, Meya Manispaa ya Morogoro ,  Mhe. Pascal Kihanga ,  ambaye pia alikuwa mgeni rasmi, ametoa wito kwa asasi mbalimbali na Taasisi za Serikali na binafsi  kuendelea kuelimisha jamii hasa kundi la vijana, kwakuwa maambukizi yanazidi kuongeza kasi kwa kundi hilo.

Meya Kihanga,  ameonesha kuchukizwa na shughuli za mtaani almaarufu kama 'vigodoro', sababu zimekuwa chanzo cha kuleta maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI,ambapo amewataka viongozi katika serikali za Mitaa kudhibiti shughuli hizo.

"Tunatambua uhuru wa watu kufurahi, lakini furaha za kutuangamiza hazitufai, popote wanapofanya haya mambo wachukuliwe hatua za kisheria"Amesema Kihanga.

Halkadhalika amekemea unyanyapaa kwa waathirika wa virusi vya UKIMWI, badala yake jamii iendelee kuwapenda, kushirikiana nao, na kuwasaidia kwa kadri inavyowezekana.

Katika hatua nyingine, Mhe.Kihanga, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau katika kuhakikisha afua zote za kupambana na virusi vya UKIMWI zinapewa kipaumbele, sambamba na kutoa utaratibu wa utoaji mikopo kwa makundi ya Vijana, Wanawake na watu wenye Ulemavu.


Mwisho amepongeza na kushukuru wadau wote walioshiriki kufanikisha maadhimisho ya siku hiyo muhimu,na kuwataka wananchi wa Manispaa ya Morogoro   kujiwekea utaratibu wa kupima afya katika kutokomeza UKIMWI ili kuishi kwa furaha.

Maadhimisho hayo yaliyobeba kauli mbiu " Chagua njia sahihi kutokomeza UKIMWI.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.