DKT. NDUMBARO AZINDUA KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA MKOA WA MOROGORO
WAZIRI wa Katiba na Sheria, Mh. Dkt. Damas Ndumbaro,amezindua rasmi Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal AID Campaign) katika Mkoa wa Morogoro.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza katika Kampeni hiyo, Dkt. Ndumbaro,amesema Kampeni hiyo ya Mama Samia inaongeza uelewa wa kisheria na haki za binadamu ndani ya jamii ikiwemo haki za wanawake na watoto, huduma ya ushauri wa kisheria na unasihi kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia pia kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu wajibu na misingi ya utawala bora.
Dkt. Ndumbaro, amewasisitiza Wananchi katika maeneo mbalimbali ambapo Kampeni hiyo itafika kujitokeza ili kupatiwa msaada wa kisheria katika masuala yanayowakabili kwani ndio lengo la kampeni hiyo.
“Lengo letu ni kuhakikisha kuwa kila Mwananchi hasa wanawake na watoto wanapata haki zao na msaada wa kisheria bila vikwazo, kampeni hii ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kuwa huduma za kisheria zinapatikana kwa wote, na kwamba wananchi wanapaswa kuwa na ujasiri wa kudai haki zao bila woga”Amesema Dkt. Ndumbaro.
Naye Mkurugenzi wa huduma za Masaada wa kisheria, Ester Msambazi, amesema Kampeni hiyo inachangia uboreshaji na upatikanaji wa haki kwa makundi mbalimbali wakiwemo wanawake, watoto na makundi mengine yaliyo katika mazingira hatarishi pamoja na kuimarisha amani na utulivu, kuongeza kipato na kuleta utengamano wa kisiasa hapa nchini.
Kampeni hiyo iliyozinduliwa rasmi Disemba 13-2024 katika eneo la stendi ya daladala ya zamani iliyopo Manispaa ya Morogoro, inaendelea kufanyika katika Halmashauri zote za Mkoa huo kwa siku 10 mfululizo ikiwa na lengo la utoaji elimu kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria kama vile Ardhi, Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mirathi, Ndoa, Ukatili wa Kijinsia, Madai, Jinai vilevile itahusisha huduma ya usajili na utoaji vyeti vya kuzaliwa na kifo vitakavyotolewa na RITA.
Post a Comment