MEYA KIHANGA AWATAKA WAZAZI KUZINGATIA LISHE BORA
MEYA Manispaa ya Morogoro , Mhe. Pasca Kihanga,amewataka Wazazi na walezi kuzingatia Lishe bora kwa watoto ili kuhakikisha wanakuwa na Afya imara ili kuepukana na udumavu.
Kauli hiyo ameitoa akiwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya afya na lishe ngazi ya Mitaa iliyofanyika Mtaa wa Misongeni 'A' Kata ya Bigwa Desemba 11-2024.
Akizungumza na Wazazi na walezi waliojitokeza kwenye maadhimisho hayo, Mhe. Kihanga, amesema lishe ndio msingi wa Afya bora kwa watoto hivyo Wazazi wanapaswa kuhakikisha elimu wanayoipata kutoka kwa wataalamu kuhusu Lishe bora wanazingatia ipasavyo.
Mhe.Kihanga, amesema lengo kuu la maadhimisho hayo ni kuweza kupata huduma za afya na lishe kufanya tathimini ya uwajibikaji wa Watendaji katika ngazi mbalimbali mfano viashiria vya utekelezaji mkataba wa afua za lishe.
" Lishe bora ni Msingi wa Maisha, Wazazi tuzingatie kuhakikisha pia watoto wetu wanapata chakula wakiwa shule ili wakue vizuri na kuweza kusoma vizuri katika kuongeza ufaulu wa masomo yao" Amesema Mh. Kihanga.
Kwa upande wa Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Lishe Manispaa ya Morogoro ,Ester Kawishe, amesema SALIKI inahusisha huduma jumuishi za kuhamasisha masuala ya afya na lishe ,upimaji wa hali ya lishe, uhamasishaji wa masuala ya kilimo na ufugaji, usafi wa maji chakula na mazingira , malezi na matendo changamshi kwa mtoto na huduma zingine za ugani.
Kawishe amesema shughuli za maadhimisho ya afya na lishe hufanyika mara moja kila robo ya mara nne kwa mwaka ambapo amesema ni muhimu viongozi wa ngazi zote wa kijamii,Watendaji ,Maafisa ugani, viongozi wa dini ,wananchi na wadau katika eneo husika kushirikishwa na kushiriki kikamilifu.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Misongeni A , Zawadi Kingo, amempongeza Meya pamoja na Menejimenti ya Manispaa ya Morogoro na Uongozi wa Kata kuadhimisha maadhimisho hayo.
Bi. Kingo, amesema kama wananchi watazingatia eleimu waliyoipata juu ya afya na lishe ,basi suala la udumavu kwa watoto litakuwa ni historia na afya za watoto zitaimarika na kuwa na afya njema.
Vilevile siku hiyo imeambatana na utoaji wa matone ya Vitamini A, upimaji wa watoto (Uzito, urefu na hali ya Lishe) pamoja na chanjo kwa watoto, na upimaji wa magonjwa mbalimbali ,mapishi kwa vitendo.
Post a Comment