Header Ads

MANISPAA YA MOROGORO YAADHIMISHA MIAKA 63 YA UHURU KWA KUPANDA MITI NA KUFANYA USAFI


WAKATI  Tanzania (zamani Tanganyika) ikiadhimisha miaka 63 ya uhuru leo Disemba 9, 2024, Manispaa ya Morogoro imeiadhimisha siku hiyo kwa kufanya usafi katika Kituo cha Afya Mafiga  na kupanda miti katika eneo hilo la Kituo cha Afya.

Tukio hilo la usafi na upandaji wa miti  limefanyika Desemba 07-2024 huku mgeni rasmi akiwa Meya wa Manispaa ya Morogoro Mhe. Pascal Kihanga.

Akizungumza na wananchi waliojitokeza katika maadhimisho  Mhe.Kihanga, amewataka wananchi wa Manispaa ya Morogoro  kuendeleza utamaduni wa kupanda miti na kutoitelekeza miti iliyopandwa ili kutunza mazingira na kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi.

Aidha, Mhe. Kihanga,  amesema kupanda miti ni muhimu katika utunzaji wa mazingira, kupata vivuli, hewa safi na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

" Tutakapokua na miti mingi katika Manispaa yetu ya Morogoro yetu itakua nzuri na mazingira yatakua mazuri hatutopata janga la njaa, upepo mkali wa kuezua majengo na hali nzuri ya hewa" Amesema Mhe. Kihanga.


Kwa upande wake, Kaimu  Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro, Christopher Komba,  amewataka wananchi wanaozunguka maeneo yaliyopandwa miti hiyo kuendelea kuitunza ila kuifanya Manispaa ya Morogoro  kua na mazingira safi na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.


Naye Diwani wa Kata ya Mafiga,Mhe. Thomas Butabile,  amewataka wananchi katika kuendelea kuenzi miaka 63 ya uhuru , wananchi waendelee kufanya usafi katika mazingira yanayowazunguka, upandaji wa miti na kuhakikisha wanashiriki shughuli  mbalimbali za kijamii kwa ajili ya Maendeleo ya Manispaa na Taifa kwa ujumla.


Katika maadhimisho hayo ,  watumishi pamoja na jamii kwa ujumla wameshiriki katika  kufanya usafi maeneo yote ya Kata ya Mafiga husani katika kufyeka nyasi  maeneo ya barabara , Ofisi za Serikali na taasisi mbalimbali.



No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.