Header Ads

MANISPAA YA MOROGORO YASAINI MKATABA WA UNUNUZI WA GREDA


KATIKA  kuhakikisha inapunguza ama kumaliza kabisa kero ya ubovu wa miundombinu ya barabara katika manispaa ya Morogoro , imeamua kununua "greda" kutokana na pesa za makusanyo ya ndani.

Akizungumza katika utiaji saini mkataba wa ununuzi wa mtambo huo Novemba 28-2024,  Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro ,Mhe. Pascal Kihanga ,  amesema kuwa lengo la kununua vifaa vyote kamili vinavyohusika na ujenzi wa barabara ili kuondoa kabisa kero za wakazi wa Manispaa ya Morogoro.

"Napenda kuwahakikishia wananchi wa Manispaa ya Morogoro kuwa tutaendelea kuendesha Halmashauri hii katika misingi ya ukweli na uwazi , nakupongeza sana Mkurugenzi kwa busara hii kwa kulifanya jambo hili kwa uwazi ili watu wajue kwa sababu watu wanataka kuona sisi tunafanya nini".Amesema Kihanga.

Mhe.Kihanga,akiwa mbele ya baadhi ya viongozi wa Menejimenti ya Manispaa  na mwakilishi  wa kampuni inayojishughulisha na uuzaji wa mitambo hiyo ya MANTRAC TANZANIA LIMITED, Collin Anamiah , amesisitiza utunzaji wa mitambo hiyo ili kuendelea kuinufaisha Manispaa hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa manispaa ya Morogoro, Emmanuel Mkongo, amewashukuru wananchi wa Manispaa ya Morogoro kwa kulipa kodi zilizowezesha ununuzi wa greda hilo.

"Greda hili Mstahiki Meya ni lao,sasa,  Manispaa ya Morogoro  tutembee kifua mbele maana mambo mazuri yanakuja, nitumie tu nafasi hii tu kuwataka wananchi wenzangu wa Manispaa ya Morogoro  kulipa kodi wasikwepe maana manufaa tunayaona".Amesema Mkongo.


Greda hilo linatarajiwa kuwasili manispaa ya Morogoro katikati ya mwezi Desemba 2024 , litakuwa mkombozi mkubwa kwa wakazi wa maeneo ambayo yana changamoto za miundombinu ya barabara katika manispaa hiyo yenye jumla ya kata 29.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.