DC KILAKALA , ATOA WITO WANANCHI KUSHIRIKI UZINDUZI WA KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA
MKUU wa Wilaya ya Morogoro,Mhe. Mussa Kilakala,amewataka wananchi wa Wilaya ya Morogoro na Mkoa mzima wa Morogoro kushiriki kwenye uzinduzi wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia ( Mama Samia Legal AID Campaign).
DC Kilakala,amezungumza hayo Ofisini kwake kwenye Mkutano wa Vyombo vya habari uliofanyika Desemba 12-2024 ambapo uzinduzi wake utafanyika Desemba 13-2024 eneo la Stendi ya Zamani ya Daladala Manispaa ya Morogoro na kuzinduliwa na Waziri wa Sheria na Katiba , Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro.
Amesema Kampeni hiyo itaanza Desemba 13-22-2024 na kufikia Halmashauri 9 za Mkoa wa Morogoro na Kata 10 na Mitaa /Vijiji 30 kwa Kila Kata ya Halmasahuri.
Aidha, DC Kilakala,amesema Kampeni imejikita katika kutoa elimu ya kisheria kwa wananchi hususan katika masuala ya ukatili wa kijinsia, migogoro ya ardhi, mirathi, usuluhishi wa migogoro kwa njia mbadala, na masuala yahusuyo haki za binadamu kwa ujumla.
Utekelezaji wa kampeni unafanyika kwa kushirikiana na Wizara na Taasisi za Serikali, Asasi za Kiraia, Wanazuoni na Wadau wa Maendeleo.
Amesema lengo kuu la Kampeni ni ni kulinda na kukuza upatikanaji wa haki kwa wote kupitia huduma ya msaada wa kisheria nchini.
Katika kufikia lengo hilo, DC Kilakala ,amesema kampeni inaongeza uelewa wa kisheria na haki za binadamu kwa jamii hususani haki za wanawake na watoto; Inatoa huduma ya ushauri wa kisheria na unasihi kwa waathirika na manusura wa ukatili wa kijinsia, kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu elimu ya sheria, masuala ya haki na wajibu na misingi ya utawala bora.
Pia,amesema Kampeni hii ni kuchangia katika kuboresha upatikanaji wa haki kwa watu wasiojiweza, hususan wanawake, watoto na makundi mengine yaliyo katika mazingira hatarishi. Vilevile, itachangia kuimarisha amani na utulivu, kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na kuleta utengamano wa kisiasa hapa nchini.
Amesema malengo mengini ni kuongezeka kwa idadi ya watu wanaotoa taarifa za matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto; kupungua kwa idadi ya migogoro na matukio yanayotokana na ukosefu wa uelewa wa sheria; Kuimarika kwa uwajibikaji na uwezo wa taasisi za Serikali na zisizo za kiserikali zinazotoa huduma za msaada wa kisheria.
Post a Comment