Header Ads

WAZIRI MKUCHIKA AWATAKA WAZAZI NA WALEZI KUSHIRIANA NA WAALIMU KUONGEZA UFAULU



WAZIRI  wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu (Kazi Maalum) Mhe. George Mkuchika amewataka wazazi na walezi  nchini kuhakikisha wanafuatilia maendeleo ya watoto wao mashuleni ili kuweza kujua changamoto  zinazowakabili na kuzitatua ili kuweza kuongeza ufaulu.

Kauli hiyo ameitoa Oktoba 26-2024  wakati akikagua ujenzi wa bweni na kuzindua madarasa mapya  shule ya Sekondari Kingolwira Manispaa ya Morogoro  ikiwa ni mwanzo wa ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Morogoro.

Mhe.Mkuchika amesema  ni wajibu  wa wazazi na walezi kushirikiana na kamati za elimu za shule za Msingi na Sekondari kuhakikisha wanafuatilia watoto wao pindi wanapokuwa shuleni ili kuweza kuwasahihisha pale wanapokosea na kuweza kuongeza ufaulu wao mashuleni.

"..Wazazi wenzangu hakikisheni mnafuatilia maendeleo ya watoto wenu mashuleni, ili kuongeza ufaulu " Amesema Mhe. Mkuchika

Aidha, Mhe. Mkuchika amesema Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea  kuweka jitihada kubwa katika kuhakikisha changamoto katika Sekta ya Elimu zinaepukika hapa nchini.

Piaamewapongeza viongozi wa Manispaa ya Morogoro kwa kutumia mapato ya ndani kujenga na kusimamia miradi na kuwaletea wananchi maendeleo.

Sambamba na hayo, Mhe. Mkuchika amesema hakuna nchi inayoendelea bila kuwepo kwa amani na upendo hivyo ni jukumu la kila Raia wa Tanzania kuhakikisha wanatunza amani na upendo kwa maslahi mapana ya Taifa.

Katika hatua nyengine Mhe. Mkuchika amewapongeza wananchi wa Mkoa huo kwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura na kuufanya Mkoa kuwa namba 3 katika uandikishaji hivyo amewataka wananchi hao kufanya kampeni za kistaarabu na kujitokeza kupiga kura Novemba 27-2024.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam  Malima amemshukuru Mhe. Rais kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na matundu ya nane choo pia ujenzi wa bweni shule ya Sekondari Kingolwira ambapo wanatarajia kuanzisha kitado cha tano na sita katika shule hiyo na kwenda kuondoa changamoto ya uhaba wa shule za (Advance level) katika Halmashauri hiyo.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Kingolwira,Shangwe Moses, amesema ujenzi wa madarasa 4 na matundu 8 ya vyoo  umegharimu jumla ya shilingi milioni 102 na laki nne pamoja na matengenezo ya viti na meza160.

Akiwa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Mkuchika amezindua madarasa manne na matundu nane ya vyoo shule ya Sekondari Kingolwira, ametembelea ujenzi wa bweni  la wanafunzi shule ya Sekondari Kingolwira, ametembelea ujenzi wa barabara ya (TACTIC) amekagua ujenzi wa Hopsitali ya Wilaya na kuzindua zahanati ya Mji Mpya ya Mji Mkuu  

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.