KAMATI YA LISHE MANISPAA YA MOROGORO YAWATAKA WAZAZI KUCHANGIA CHAKULA SHULENI
KAMATI ya Lishe Manispaa ya Morogoro imetoa elimu ya umuhimu wa huduma ya utoaji chakula shuleni ili kuboresha lishe ya wanafunzi na kuinua kiwango cha ufaulu.
Elimu hiyo imetolewa Oktoba 28-2024 ikiwa ni muendelezo wa utoaji elimu kwa kila robo ya mwaka wa fedha pamoja na maandalizi ya Siku ya Lishe duniani.
Akizungumza mara baada ya ziara hiyo,Kaimu Mwenyekiti wa Kamati,ambaye ni Mchumi wa Manispaa ya Morogoro, Edward Mwamotela, amesema kuchangia chakula cha wanafunzi shuleni kunasaidia kulinda haki ya mwanafunzi ya kupatiwa huduma muhimu na kuongeza kiwango na ufaulu na hatimaye kupata wataalam wa kuendeleza taifa.
Mwamotela, amesema, mpango wa utoaji huduma ya chakula shuleni unalenga kuleta matokeo chanya, kwani bila kufanya hivyo ni kuwatesa watoto wanaotoka nyumbani asubuhi na kurudi jioni bila kupata chakula huku watoto waliobaki majumbani wakipata milo kamili asubuhi na mchana.
“Ni mateso makubwa na ni dhambi mbele za Mungu kushindwa kuwachangia chakula watoto wetu ambao Mungu ametujalia kama baraka, natoa wito kwa wazazi kuendelea kuchangia chakula shuleni,hii iwe ajenda ya kudumu shuleni,kwani watoto wakipata chakula watakuwa na uelewa mzuri na hatimaye kuongeza ufaulu darasani na kutengeneza kizazi chenye afya bora" Amesema Mwamotela.
Kwa upande wa Mkuu wa Divisheni ya Afya,Lishe na Ustawi wa Jamii Manispaa ya Morogoro,Dkt.Maneno Focus ,amesema Divisheni ya Afya inaendelea kusimamia suala la lishe na utekelezaji wa agizo la Rais lakini pia inaendelea kutoa elimu ya usafi wa afya na mazingira katika maeneo mbalimbali huku akitoa rai kwa watendaji kuendelea kuhamasisha suala la usafi wa mazingira kwa wananchi katika maeneo mbalimbali ikiwemo majumbani na maeneo ya biashara ili kujiepusha na magonjwa ya mlipuko ikiwemo ugonjwa wa kipindupindu.
Naye Mkuu wa Kitengo cha huduma za Lishe Manispaa ya Morogoro,Ester Kawishe, amesema ni wakati sasa wa wazazi kuamka na kuunga mkono suala la lishe shuleni ili kumpa mwanafunzi utulivu wa akili na nguvu ya kusoma na kuelewa vyema.
Post a Comment