Header Ads

MAADHIMISHO SIKU YA WAZEE DUNIANI YAFANA,RC MALIMA ATOA WITO MKALI KWA WANAOCHEZA NA STAHIKI ZA WAZEE



MANISPAA ya Morogoro imeadhimisha siku ya wazee duniani huku Mkuu wa Mkoa wa Morogoro akitoa maagizo mazito kwa viongozi wa Serikali juu ya huduma na stahiki za wazee.

Maadhimisho hayo yamefanyika Makazi ya wazee Fungafunga Oktoba 01-2024 ambapo mgeni rasmia akiwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro,Mhe.Adam Malima.

Akizungumza na Wazee pamoja na wananchi ,RC Malima,amesema lengo la hafla hizi ni kuelimisha jamii haki na stahili mbalimbali zinazohitajika kwa wazee hao sanjari na kuwakumbusha wazee umuhimu wa uwepo wao katika jamii husika.

RC Malima,amesema serikali inatambua umri wa mzee ni kuanzia miaka 60 na kuendelea na kwamba kila mmoja anapaswa kutambua kuwa siku moja ataufikia uzee hivyo wazee wanapaswa waheshimiwe,watunzwe na kuenziwa.

“Nawasihi tutumie hekima na ushauri walionao wazee wetu na siyo kuanza kuwafanyia vitendo vya ukatili kwa kuwanyanyasa,kuwatenga na kuwaua kwa imani potofu,na serikali itaendelea kuchukua hatua kali za kisheria kwa watakaonyanyasa wazee kwa namna yoyote ile”Amesema RC Malima.

Katika hatua nyingine aliziagiza halmashauri za Mkoa wa Morogoro  ambazo hazijatekeleza zoezi la kutambua wazee na kuwapatia kadi za matibabu bila malipo pamoja na kutimiza matakwa yote ya stahiki za wazee.

"Kama kuna eneo ambalo kwangu litanikwaza ni kuchezea wazee,nawaagiza Wakurugenzi wote hakikisheni stahiki za wazee mnaizitekeleza ,kwani stahiki zao sio ombi ni lazima, na maafisa Tarafa na Kata kama nikija kwenye eneo lako harafu huna taarifa sahihi ya wazee hilo ni balaa lengine" Ameongeza RC Malima.

Aidha,RC Malima, amewahakikishia wazee kuwa mkoa wa Morogoro utaendelea kuhakikisha kuwa dawa zote za magonjwa ya wazee zinapatika kwenye vituo afya huku akiwataka wakurugenzi wa halmashauri kufanya ukaguzi wa dawa na fedha kwa kila robo ya mwaka.

Kuhusu suala la miundombinu ya barabara ,amesema tayari mkandarasi amepatikana na zaidi ya milioni 400 zimetengwa kwa ajili ya barabara na daraja ili kurahisisha huduma ya kufika katika makao hayo pamoja na maeneo mengine ya Taasisi na wananchi.

Maadhimisho ya siku ya wazee duniani Manispaa ya Morogoro yameenda sambamba na uzinduzi wa Jengo la Bwalo la kisasa la Makazi ya kulelea wazee Fungafunga.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.