Header Ads

DC KILAKALA ALITAKA BARAZA LA MADIWANI MANISPAA YA MOROGORO KUTILIA MKAZO UPATIKANAJI MADAWATI SHULENI






MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Mussa Kilakala,amelitaka Baraza la Madiwani Manispaa ya Morogoro kutilia mkazo suala la upatikanaji wa madawati shuleni.

Kauli hiyo ameitoa katika Baraza la Kawaida la Madiwani la robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024-2025 lililofanyika Ukumbi wa Manispaa ya Morogoro.

Akizungumza katika baraza hilo, DC Kilakala,amesema ni aibu kwa Manispaa watoto kukaa chini kwani Manispaa ndio kitovu cha Mkoa wa Morogoro.

"Madiwani hili suala la madawati lipeni kipaumbele sana, hakikisheni katika bajeti zenu tengeni fedha za kutosha za kununua madawati,sisi ni kitovu cha Mkoa, lazima wapiga kura wetu tuwahurumie kwa watoto wetu , najua mna vipaumbele vingi lakini suala la Madawati lichukue nafasi kubwa watoo wetu wasome katika mazingira rafiki" Amesema DC Kilakala.

Aidha,amesema atahakikisha anawakutanisha wadau wa maendeleo kuona namna ya kuchangia suala la madawati.

Hata hivyo, DC Kilakala, ameipongeza Manispaa ya Morogoro kwa kushiriki kikamilifu na kufanya vizuri katika zoezi la uandikishaji la wapiga kura huku akiwataka waendelee na hamasa ya kuhakikisha wananchi wanajitokeza kwa wingi kupiga kura Novemba 27-2024.

Upande wa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Morogoro Mjini, Fikiri Juma,ameitaka Manispaa ya Morogoro kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato ili kufikia ndoto yake ya kuwa Jiji 

Meya wa Manispaa ya Morogoro,Mhe. Pascal Kihanga,amesema katika Bajeti zinazoendelea atahakikisha wanatenga fedha za kutosha kwa ajili ya kuongeza madawati.

"Manispaa tunavipaumbele vingi katika bajeti, lakini hili la DC tunaenda kulifanyia kazi, tayari ile adhima yetu ya kuwa na greda letu la kuchonga barabara linatimia kinachofuatia ni kuongeza nguvu katika vipaumbele vyengine" Amesema Meya Kihanga.

Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro,Emmanuel Mkongo,amesema yote ambayo yametolewa kama ushauri kwa kushirikiana na menejimenti yake watayafanyia kazi ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi wa manispaa ya Morogoro.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.