MANISPAA YA MOROGORO YATOA MAFUNZO KWA WASIMAMIZI WA MIKOPO YA ASILIMIA 10 NGAZI YA KATA,ZAIDI YA MILIONI 827 ZIMETENGWA KUTOLEWA
MANISPAA ya Morogoro imeendesha mafunzo kwa wataalamu na wasimamizi wa Mikopo ngazi ya Kata yanayolenga kuwajengea uwezo wa kusimamia utoaji wa Mikopo ya 10% ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu Walemavu.
Akizungumza na wataalamu hao, Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Morogoro, Faraja Maduhu, amesema lengo Kuu la Mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo Wataalamu ambao wataenda kutoa Elimu na hamasa kwa Jamii juu ya uundaji Vikundi vyenye sifa ya kupata huduma hiyo ya Mikopo lakini pia kusimamia marejesho ya Mikopo hiyo.
Maduhu,amesema Manispaa ya Morogoro kipindi cha mwaka wa fedha 2024-2025 katika robo ya pili imetenga jumla ya milioni 827,022,718.41 .kwa ajili ya kutoa mikopo ambayo inatarajia kuanza kutolewa Novemba 2024.
"Serikali imeamua kurejesha mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu iliyokuwa imesitishwa hapo awali , kwahiyo kwa mafunzo haya tunaamini timu zenu za wataalamu mtaenda kufanya kama miongozo ya utoaji hii mikopo inavyotaka, niwaombe wataalamu wetu, nendeni mkachakate vikundi vyenu ili muone vikundi gani vyenye sifa muweze kuvipatia mikopo" Amesema Maduhu.
“Mikopo hii ilisimama mwaka jana lakini mwaka huu 2024 tumekuwa na muongozo mpya wenye kanuni mpya hivyo tunapitia muongozo pamoja na kanuni zote ili wasimamizi hawa wawe tayari kwa ajili ya kuhamasisha vikundi, kuunda vikundi pamoja na kuwaongoza katika suala zima la kuomba mikopo hii ambayo ni asilimia 10 za mapato zinazotengwa na halmashauri" Ameongeza Maduhu.
Aidha,Maduhu,amesema baada ya Mafunzo haya, Wataalamu wataenda kufanya mikutano katika Kata zao kuhamasisha Jamii kuanzisha Vikundi vitakavyoweza kunufaika na Mikopo ya 10% ya mapato ya Halmashauri. makundi haya ya Wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu.
Post a Comment