Header Ads

MANISPAA YA MOROGORO YAZINDUA KAMPENI YA SOMA NA MTI MASHULENI, YAANZA NA SUA NA MBUYUNI KWA KUPANDA MITI 1000

 







MANISPAA ya Morogoro, imezindua  kampeni kabambe ya upandaji miti katika shule huku akibainisha kuwa wamepanga kupanda miti zaidi ya milioni 1 na laki 5  kupitia wanafunzi wa shule za msingi,sekondari na Vyuo  na maeneno ya wananchi na pembezoni mwa vyanzo vya maji.

Uzinduzi huo umefanyika leo Februari 25/2022 ukijumuisha Shule mbili za Sekondari ikiwamo Mbuyuni na SUA ambapo miche hiyo imefadhiliwa na Shirika la SAT wadau wakubwa wa maendeleo hususani katika utunzaji wa mazingira.

Akizindua Kampeni hiyo yenye kauli mbiu ya “Soma na mti”  Afisa Mazingira Manispaa ya Morogoro, Samwel Subby,  amesema lengo la kuzindua Kampeni hiyo Mashuleni ni kuhakikisha Wanafunzi waone zoezi la upandaji miti ni sehemu ya maisha ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi. 

" Tumezindua Kampeni hii katika Shule ya Sekondari  Mbuyuni na SUA, tunawashukuru wadau wetu SAT kwa kutupatia miche 1000 ambayo tumeipanda leo, tunashukuru Viongozi wa Kata, vyama vya Siasa, wadau wote wa Mazingira , wananchi  na  wanafunzi, kampeni hii ili ifanikiwe tunataka kila  mwanafunzi apande mti mmoja na huo mti atatutunza hadi atakapomaliza shule, nitoe rai kwa Wananchi kampeni hii isiwe mashuleni bali kila mtu apande miti katika maeneo yao na kila Taasisi ipande miti ili tuweze kukabiliana na Tabianchi" Amesema Subby.

Subby, amewaagiza maafisa afya na Mazingira ngazi ya Kata kuhakikisha wananchi  wanafanikisha upandaji wa miti milioni 1 na laki 5 ambayo Manispaa ya Morogoro imejiwekea  ili kukabilianana mabadiliko ya tabia nchi

Aidha, Subby,  amewaagiza Maafisa Afya na  Mazingira ngazi za Kata  kuisimamia kampeni hiyo kwa kwenda mashuleni na vyuoni kuikagua miti hiyo ambayo itakuwa imepandwa.

Mwisho, Subby, ameagiza kufufuliwa kwa  Klabu za utunzaji  wa mazingira katika shule pamoja na Maafisa elimu kuisimamia kwa vitendo  kampeni ya soma na mti kuhakikisha inatekelezwa kikamilifu.

Naye , Balozi wa Mazingira Tanzania kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais na Mwakilishi wa Moro Kwanza Mazingira, Chage,  amesema ukosefu wa mvua unasababishwa na mabadiliko ya tabia nchi hivyo kuna wajibu wa kuhakikisha mazingira yanatunzwa ikiwa ni pamoja na miti kupandwa.

Diwani wa Kata ya Mbuyuni, Mhe. Samwel Msuya,  ameishukuru Manispaa na wadau kuzindua Kampeni hiyo katika Kata yake , huku akiwataka  wale wenye viwanja vipya kupanda miti mitatu katika viwanja hivyo   ikiwemo wa kivuli na mti mmoja miwili ya matunda huku akidai kwamba agenda ya utunzaji wa mazingira katika Kata ya Mbuyuni iwe endelevu.

Naye,mwanafunzi wa kidato cha kwanza, Elizabeth Ngonyani, ameiomba  jamii na wanafunzi kusimamia kampeni hiyo ili ifanikiwe huku akiiomba serikali kuwachimbia kisima ili kurahisisha upatikanaji wa maji ya kutunza miti inayopandwa.

Shule ya Mbuyuni ni shule ya kwanza ambayo itaanzishwa shamba la Vitalu vya miche ya miti ya vivuli na matunda ikiwamo na maua ili kuwa mfano kwa shule nyengine lengo likiwa ni kuzalisha miche zaidi katika kusaidia kampeni hiyo.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.