Header Ads

CCM KATA YA MAFIGA WAADHIMISHA MIAKA 45 YA CCM KWA KUPANDA MITI ZAIDI YA 500 KATIKA SHULE ZILIZOPO KATA YA MAFIGA.

 

Diwani wa Kata ya Mafiga, Mhe. Thomas Butabile, akipanda mti katika Shule ya Sekondari Mafiga.


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mafiga Manispaa ya Morogoro, kimeadhimisha miaka 45 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa upandaji wa miti.

Zoezi hilo la upandaji wa miti limezinduliwa leo Februari 04/2022 katika Shule ya Sekondari Mafiga.

Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, Diwani wa Kata ya Mafiga, ambaye ndiye mgeni rasmi, amesema lengo la kupanda miti katika shule ni kuhakikisha kuwa shule zote zinakuwa na mazingira mazuri na yenye ukijani.

Mhe. Butabile, amesema kuwa ,shule zilizopo katika Kata yake bado hazirishishi kimazingira jambo ambalo limewafanya kuelekeza nguvu katika kupanda miti.

“Leo tumepanda miti Zaidi 500, chama chetu kimefanya maadhimisho haya kwa kupanda Zaidi ya miti 500 kwa shule zetu zote 5 lengo likiwa ni kutunza mazingira , lakini pia niwaombe wana CCM na Waalimu kwa pamoja tuendelee kumuunga mkono Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan kwani tunaona mambo makubwa anayofanya katika muda mfupi ambao yupo madarakani ,tumeona ametupa fedha za ujenzi wa madarasa ya UVICO-19 , ili wanafunzi wetu wasome katika mazingira rafiki ” Amesema Butabile.

Naye Mwakilishi wa Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mafiga, Hamis Lyoba, amesema matarajio yao ni kuona  miti hiyo inatunzwa.

Kwa upande wa Katibu wa CCM Kata ya Mafiga,Farida Rajabu, amewataka wenyeviti na viongozi wa jumuiya kutenga muda kwa ajili ya ufuatiliaji wa miti hiyo.

Shule zilizopanda miti hiyo ni pamoja na shule za Msingi Mafiga A na B, Misufini A na B na shule ya Sekondari Mafiga.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.