TARURA YATOA ELIMU YA MFUMO WA MAEGESHO KIDIGITALI KWA VIONGOZI WA HALMASHAURI YA MANISPAA YA MOROGORO
MAMLAKA ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wametoa taarifa elekezi ya kuwajengea uwezo na Kutoa elimu kwa Viongozi wa Halmashauri ya manispaa ya Morogoro, Madiwani, Wakuu wa idara na vitengo pamoja na Wawakilishi wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama wa Wilaya kuhusu mfumo mpya wa Kielektroniki wa malipo ya Ushuru wa maegesho ya magari.
Taarifa hiyo imetolewa katika Mkutano maalumu
wa baraza la madiwani manispaa ya morogoro katika kupitisha bajeti ya mwaka wa
fedha 2022/2023.
Mfumo wa Maegesho Kidigitali (TeRMIS) ni mfumo wa Kielektroniki
wa usimamizi na ukusanyaji wa mapato yatokanayo na maegesho ya vyombo vya moto
(parking fee), matumizi ya Hifadhi za barabara (Road Reserve User Charges)
pamoja na Adhabu kutokana na Ukiukwaji wa matumizi ya hifadhi za barabara.
Mfumo huu wa Kidigitali unampa muda mtumiaji wa maegesho kulipia
Ushuru wa Maegesho ndani ya Siku 14 tangu alipotumia Maegesho na endapo atashindwa
kulipa ndani ya muda huo atatakiwa kulipa Ushuru wa Maegesho pamoja na faini ya
Shilingi 10,000/=.
Kwa Mkoa wa Morogoro, mtumiaji wa maegesho atatakiwa kulipa
Shilingi 300 kwa Saa na Shilingi 1,000 kwa Siku.
Mfumo wa Maegesho Kidigitali unadhibiti mianya ya upotevu wa
mapato ya Serikali kwani umeunganishwa na mfumo wa GePG ambapo Mtumiaji wa
maegesho anapaswa kulipia ushuru wa maegesho baada ya kupatiwa kumbukumbu namba
ya malipo (control number) na atatumia kumbukumbu namba hiyo kulipia maegesho
kwa kutumia mtandao wowote wa simu ya mkononi, Benki ya NMB na CRDB au kupitia
kwa Mawakala wa Huduma za fedha.
Lengo ni kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa
mapato ya serikali yatakayosaidia kuboresha miundombinu ya barabara zote nchini.
Post a Comment