WANAKIKAPU TUNASIKITIKA KUMPOTEZA MWANAKIKAPU MAHIRI EPHRAIM KIBONDE
Shirikisho la mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) linatoa salamu nyingi za pole kwa Wazazi, Watoto, ndugu, jamaa na wana familia wote wa Marehemu Ephraim Kibonde, salamu za pole kwa Clouds Media Group, Wanahabari na wanamichezo wote nchini kutokana na msiba mkubwa wa Mwanakikapu mwenzetu Ephraim ambaye alikuwa ni Mtangazaji nguli wa habari na michezo nchini na muongozaji mahiri wa shughuli (MC).
Marehemu Ephraim alianza kucheza kikapu akiwa mdogo, alikuwa mchezaji nyota wa kikapu katika Shule ya sekondari Mzizima na alipomaliza shule alijiunga na kituo cha vijana cha Don Bosco ambapo alicheza katika timu ya Don Bosco youth centre upanga na mnamo mwaka 1992 alikuwa katika timu iliyoshiriki daraja la pili na baadae mwaka huo alifanikisha timu hii kupanda daraja la kwanza.
Katika michezo aliyocheza marehemu mchezo muhimu ambao unakumbukwa sana timu yake ilicheza dhidi ya timu ya Risasi ya Shinyanga ambapo Marehemu Ephraim alitoa pasi ya mwisho (assist) kwa mchezaji Dk. Peter Maro ambaye alirusha na kufunga point 3 na kuipandisha timu yao daraja.
Kwa sehemu kubwa safari ya mafanikio ya maisha ya marehemu Ephraim yalianza kwenye kikapu ambapo itakumbukwa kuwa Ephraim alishiriki katika kamati mbalimbali za maandalizi ya matamasha ya Don Bosco Youth festivals. Sehemu kubwa aliyoshiriki katika hizo kamati ni katika kitengo cha habari kama Muongoza shughuli (MC).
Na hata safari yake yake ya utangazaji ilianzia katika mchezo wa kikapu, wakati ule akiwa pale Don Bosco alikuwa anafanya kazi ya kuwa MC na kwenye moja ya sherehe ya kufunga mashindano pale Don Bosco, mmoja wa wageni alikua ni Mkurugenzi wa kampuni ya Televisheni ya CTN ambapo alivutiwa sana na utangazaji wa Ephraim na ndipo aliongea na Fr. Peter Paul kumtaka Ephrahim kwenda ofisini kwake.
Hapo ndio ikawa mwanzo wa maisha ya utangazaji kwa Ephraim na yalitokana na mafanikio ya kituo cha Vijana cha Don Bosco Upanga kupitia matamasha na mchezo wa kikapu.
Marehemu Ephrahim katika maisha yake licha ya kuwa mchezaji wa Kikapu wa timu za Sekondari Mzizima na baadae Kituo cha Don Bosco Upanga pia alishawahi kuwa mmoja wa Wakurugenzi katika chama cha Mpira wa Kikapu mkoa wa Dar es Salaam (BD) chini ya Rais wa wakati huo wa BD Simon Msofe na Mkurugenzi Mtendaji marehemu Mbamba Uswege.
Marehemu Ephraim hadi anafariki alikuwa bado ni mchazaji wa kikapu kwa timu ya wachezaji wa zamani ambao walikuwa wakifanya mazoezi walau mara moja kwa juma, pia Marehemu Ephraim atakumbukwa mwaka jana mwishoni alicheza mchezo wa Kikapu wa Tigo Fiesta Basketball Bonanza kati ya Wafanyakazi wa Clouds Media Group na Wasanii na alionyesha umahiri mkubwa katika mchezo huo uliofanyika katika viwanja vya Gymkhana, Dar es Salaam.
Marehemu Ephraim anakumbukwa kwa uchambuzi mahiri wa mchezo wa kikapu nchini hasa ligi za RBA, NBL, Taifa Cup, NBA na utangazaji wa michezo mingine mbalimbali kama soka, masumbwi, riadha n.k.
Kama shirikisho mpira wa Kikapu Tanzania tutaendelea kumuenzi Marehemu Ephraim Kibonde kwa kuhakikisha kuwa tunaundeleza mchezo huu wa kikapu nchini kote ili uweze kufungua fursa kwa Watanzania wengi zaidi kama ambavyo yeye Marehemu aliipata kupitia Kikapu.
Tunaomba wadau wa maendeleo tushirikiane ili kuendeleza mchezo wa kikapu nchini Tanzania ili tufungue fursa zaidi kupitia mchezo wa kikapu ili kusaidia maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa Watanzania wengi hususani vijana nchini kote.
Tunaomba wote tuendelee kuwaombea Wazazi wa marehemu na zaidi watoto wa Marehemu ili Mungu awe mfariji wao kipindi hichi kigumu cha kumpoteza Mpendwa wao Ephraim.
Bwana alitoa na Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe, tunaomba Mungu amlaze mahala pema peponi Marehemu Ephraim Kibonde, Amina.
Phares Magesa
Rais,
Shirikisho la mpira wa kikapu Tanzania (TBF)
www.tbf.or.tz
Post a Comment