Header Ads

KAMATI YA HUDUMA ZA UCHUMI , ELIMU NA AFYA YAPONGEZA UJENZI MIRADI YA ELIMU NA AFYA KUKAMILIKA KWA WAKATI.









KAMATI ya Huduma za Uchumi, Elimu na Afya Manispaa ya Morogoro imepongeza wataalamu pamoja na timu nzima ya Utawala ikiongozwa na Mkurugenzi wa Manispaa kwa kukamilisha miradi ya elimu na afya  kwa wakati , ikiwemo ujenzi wa madarasa ya Pochi la Mama.

Pongezi hizo zimetolewa Januari 19/2023 na kamati hiyo  iliyoongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kingo, Mhe. Amini Tunda baada ya kukagua ujenzi wa madarasa ya shule za Sekondari na Msingi pamoja na miradi ya afya.

Akizungumza katika ziara hiyo juu ya ujenzi wa madarasa, Mhe. Tunda, amesema Manispaa ya Morogoro ilipokea Shilingi Bilioni 1.6 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 81 kupitia  fedha zijulikanazo kama Pochi la Mama ikiwa na lengo la kuinua kiwango cha taaluma na kufuta machaguo ya kwanza, pili na tatu kama ilivyozoeleka hapo awali.

Amesema Serikali inawajali wananchi wa Manispaa ya Morogoro  na kwamba wameitendea haki fedha ya Serikali lakini pia wamekamilisha kwa wakati na kazi yao kuwa nzuri hali inayoashiria hakuna hata mwanafunzi mmoja ambaye atashindwa kuwasili darasani na kuanza masomo kutokana na uhaba wa madarasa kwenye halmashauri hiyo.

Pia, Wajumbe wa Kamati hiyo wamepongeza  timu ya Utawala ya Manispaa inayoongozwa na Mkurugenzi wa Manispaa, Ally Machela,  kwa kuongeza madarasa  2 kupitia mapato ya ndani  na kuongeza madarasa katika fedha ya pochi la mama na kufanya jumla ya madarasa 83 jambo ambalo limeonesha jinsi gani Manispaa imeunga mkono juhudi za Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ,  za kuboresha elimu kwani kazi za mapato ya ndani ni kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Mhe. Tunda, amesema kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Manispaa ya Morogoro kupitia mapato yake ya ndani kwa kipindi cha mwezi mmoja iliweza kukamilisha ujenzi wa madarasa 10 lengo likiwa ni kuongeza nguvu kwenye ujenzi wa madarasa.

Mwisho kamati hiyo, imeipongeza Menejimenti ya Manispaa kwa hatua nzuri ya Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya , kukamilisha ujenzi wa Zahanati 6 ambazo zote zimeanza kutoa huduma , ujenzi wa Vituo vya afya 2, Lukobe na Tungi ambavyo vipo katika hatua ya mwisho pamoja na Zahanati mpya ambazo ujenzi unaendelea.

Upande wa Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Jeremia Lubeleje, ameipongeza Serikali chini ya Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, .Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoa fedha nyingi ili kujenga madarasa , ambapo awali aliipatia Manispaa Shilingi Bilioni 1.7 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 86 ya UVIKO-19.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.