JUMUIYA YA WAZAZI CCM WILAYA YA MOROGORO MJINI YAADHIMISHA MIAKA 46 YA CCM KWA KWA KUPANDA MITI ENEO LA MRADI WA BWAWA LA SAMAKI .
JUMUIYA Wazazi Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Morogoro Mjini, imeadhimisha Miaka 46 ya CCM kwa kutembelea na kukagua eneo la Mradi wa bwawa lao la Samaki ikiwa ni pamoja na upanda miti katika eneo hilo.
Mbali ya kutembelea eneo la miradi wa Bwawa la Samaki , pia wamepanda miti shule ya Msingi Konga sambamba na kuzungumza na wanachama wa CCM Kata ya Mzinga waliojitokeza katika zoezi la upandaji wa miti.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo yaliyofanyika Januari 28/2023 katika eneo la Ofisi ya Kata ya Mwembesongo, Mgeni rasmi kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini, Mhe. Dkt. Mohamed Abood, Katibu wa CCM Wilaya ya Morogoro Mjini , CDE. Amiri Mkalipa, ameipongeza Jumuiya ya Wazazi kwa maandalizi mazuri pamoja na kazi kubwa wanazozifanya za kuimarisha uhai wa Jumuiya.
"Hii ndio Jumuiya ninayoitaka, tunataka tufanye kazi, Mhe. Rais ameruhusu mikutano ya hadhara, ni muda wa kukisemea Chama na kusema yale yanayofanywa na Rais katika kuiletea maendeleo Tanzania" Amesema Mkalipa.
" CCM ni chama kinachotetea wanyonge, viongozi tusiwe sehemu ya kero, tukawa watu wa kulalamika tu badala ya kutatua kero za wananchi, kama jambo lipo ngazi ya tawi litatuliwe kwenye ngazi ya tawi badala ya kusubiri viongozi wa ngazi za juu kuja kutatua”,Ameongeza Mklaipa.
Naye Mwenyekiti wa Wazazi CCM Wilaya ya Morogoro Mjini, Salum Kipira, amwaomba wana ccm kuendeleza umoja na mshikamano kwani uchaguzi umeisha sasa ni wakati wa kufanya kazi.
" Kila aliye na dhamana ya uongozi tumpe nafasi aongoze. Napenda tuwe wamoja ili tutekeleze tuliyopanga, sitavumilia migogoro, kama upo kwenye Jumuiya yetu unatukwamisha hatutakuvumilia”Amesema Kipira.
" Nisisitizie hili, kila Viongozi na wana jumuiya ya Wazazi na wana ccm tunao wajibu kama wazazi wa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa kuwafichua wahalifu wanaoharibu watoto, na wanaowafanyia watoto vitendo viovu,Sasa hivi maadili yameharibika, watoto wanabakwa na wanalawitiwa,mbaya zaidi wazazi wanapokea pesa kesi zinamalizwa kienyeji”,Amesisitizia Kipira.
Naye Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Morogoro Mjini, Ruth Mutashaba, amehamasisha jamii kupeleka watoto shule badala ya kuwaozesha huku akieleza kuwa CCM itafanya ziara ya kuwasaka watoto waliopewa mimba na kuachishwa masomo na kuwabaini wahalifu.
Katika maadhimisho hayo zaidi ya kadi 1000 zimegaiwa kwa wanachama wapya waliojiunga na Jumuiya ya Wazazi.
Post a Comment