Header Ads

WANUFAIKA WA MIKOPO ISIYO NA RIBA WATAKIWA KUFANYA MIRADI YENYE TIJA ILI KUWEZA KUFANYA MAREJESHO.



WANUFAIKA  wa mikopo isiyo na riba ya asilimia 10 ya mapato ya ndani inayotolewa na halmashauri kwa vikundi vya vijana, wakina  mama na watu wenye Ulemavu  Manispaa ya Morogoro wametakiwa kufanya shughuli za uzalishaji zenye tija na zitakazoleta faida ili kupata faida na kumudu kurejesha mikopo hiyo.

Rai hiyo imetolewa Desemba 29/2022 kwenye Ukumbi wa Mikutano Ofisi Kuu na Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Faraja Maduhu, wakati wa kufungua mafunzo kwa wawakilishi 87 ambao ni Makatibu , wenyeviti na waweka hazina wa Vikundi 29 vinavyotakiwa kupata mikopo kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Akizungumza na wanavikundi hivyo, Maduhu,  amebainisha kuwa ni vema kila kikundi kujikita kwenye shughuli za mradi ambao mmewasilisha kwenye andiko na kusimamia mradi huo ili uweze kuleta faida kwa manufaa ya familia na kurejesha deni pia.

Maduhu, amesema kuwa, ni muhimu kila mwanakikundi kutambua masharti ya mkopo unaotolewa na Serikali ya Awamu ya sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kuwajibika ipasavyo kufanya shughuli za miradi iliyokusudiwa ili fedha hizo ziweze kurudishwa kwa wakati na kusisitiza utunzaji wa kumbukumbu za matumizi yote ya fedha ili kuepuka upotevu wa fedha za Serikali.

“Mikopo hii inatolewa kwa watu waliokidhi vigezo kulingana na kiasi cha fedha kilichopo na si vinginevyo, ninyi mna sifa na mmekidhi vigezo vya kupata mkopo huu, niwaombe kuepuka matumizi yoyote yasiyo ya lazima ili muweze kufikia malengo yenu na kurejesha fedha hizo kwa wakati.” Alisisitiza Mvaa.

Naye Afisa Maendeleo ya Jamii , ambaye ni mwezeshaji wa elimu ,Joyce Mugambi,  amesema kuwa lengo la Serikali kutoa mikopo hiyo isiyo na ribariba, walemavu, vikundi vya vijana na akinamama ni kutoa fursa kwa jamii kuinuka kiuchumi kupitia shughuli mbalimbli za uzalishaji ikiwa ni pamoja na kuzakuza ajira hasa kwa vijana ambao wanapitia changamoto ya kukosa mitaji ya kuanzisha biashara.

Kwa upande wa Mwezeshaji mwengine kutoka Idara ya Maendeleo ya Jamii, Josephine Mkuli, amesema Fedha hizo sio kwa ajili ya kugawana kwa kila mwanakikundi na kila mtu kufanya mradi anaotaka bali ni kwaajili ya kufanya mradi uliokusudiwa na wanakikundi wote kwa pamoja na faida itakayopatikana ndiyo inapaswa kugawanywa kwa kila mwanakundi.

wanufaika hao wameishukuru Serikali ya Awamu ya sita, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali, wananchi wake na kuwapatia fursa nyingi za kujikwamua kiuchumi pamoja na kuzalisha ajira kwa watanzania waliokuwa wamekata tamaa ya kujiendeleza, kiuchumi kutokana na kukosa mitaji ya kufanyia biashara.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.