Header Ads

MANISPAA YA MOROGORO YAADHIMISHA MIAKA 61 YA UHURU, MSULWA AHIMIZA WANANCHI KULINDA AMANI.

 

MANISPAA ya Morogoro imeadhimisha  sherehe za miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania Bara kwa kuandaa Kongamano la kujadili Maendeleo Endelevu ambayo Manispaa imeyapata katika kipindi cha Miaka 61  ya uhuru.

Kongamano hilo limefanyika Desemba 09/2022 katika Ukumbi wa Mikutano Ofisi Kuu ya Manispaa ambapo mgeni rasmi akiwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa ambaye ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa Kongamano hilo.

Akizungumza  katika kongamano hilo, Mhe. Msulwa,  alieleza kuwa ratiba hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.  Samia Suluhu Hassan kwa mikoa na wilaya zote kuadhimisha sherehe za miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania Bara kwa kuandaa makongamano.

Katika Kongamano hilo, Mhe. Msulwa, amehimiza Wananchi kudumisha umoja  na kulinda amani ya nchi kwa maendeleo Endelevu.

Msulwa, amesema kuwa,Tanganyika ilipata Uhuru Mwaka 1961 kwa amani bila umwagaji damu,hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kuilinda amani ya nchi na kudumisha umoja ili nchi yetu iwe na maendeleo endelevu.

Naye Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Ruth John, amesema Kongamano hilo limelenga kuwakumbusha wananchi kuwa wanapaswa kujivunia amani waliyonayo kwani katika kipindi chote tangu kupatikana kwa uhuru hakujawahi kutokea machafuko kama ilivyo kwa maeneo mengine.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, amesema katika kipindi cha miaka 61 ya Uhuru Manispaa inaendelea kukua kwa kasi kwani miradi mingi imekuwa ikitekelezwa kupitia fedha za ruzuku na fedha za mapato ya ndani.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Ally Machela,  amesema Manispaa itaendelea kutoa huduma bora kwa wananchi na kuimarisha pamoja na kuoboresha huduma zote muhimu ikiwamo huduma ya Maji, Umeme,  Miundombinu ya afya na Barabara ,  Masoko pamoja na huduma za kijamii.

Katika hatua nyengine, aliyekuwa Katibu wa kwanza wa TANU Mkoa wa Morogoro, Mzee Juma Salumu Digallu, aliwashukuru waandaji wa  kongamano hilo na kusema limewakumbusha wapi wametoka na wapi walipo na kuipongeza serikali kwa jitihada kubwa inayofanya kuleta maendeleo nchini.

Digallu, ameshauri Manispaa kuweka alama yoyote itakayotambulisha kuenzi mchango wa Mwalimu Nyerere katika kupigania maendeleo ya Mkoa wa Morogoro kwa kuanzisha Viwanda vilivyokuwa ni sehemu ya ajira ya wananchi wa Morogoro akiwa Mbunge wa Kwanza wa Jimbo la Morogoro Mjini .

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.