MANISPAA MOROGORO YAADHIMISHA SIKU YA UKIMWI DUNIANI, DAS MOROGORO AWAASA WANANCHI WAISHIO NA VVU KUENDELEA KUTUMIA DAWA ZA KUFUBAZA VIRUSI.
KATIBU Tawala Wilaya ya Morogoro ,Ruth John akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Morogoro katika maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani Manispaa ya Morogoro, amewaasa Wananchi wanaoishi na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kuendelea kutumia dawa za kufubaza virusi hivyo ili waweze kuishi maisha yenye afya na amani wakati wote.
Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wananchi waliojitokeza katika Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani Manispaa ya Morogoro iliyofanyika Desemba 01/2022 katika Viwanja vya Chuo cha Mifugo Liti Kata ya Mlimani.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Bi. Ruth , ameipongeza Manispaa ya Morogoro , wadau wa Ukimwi na kamati kwa kuandaa siku muhimu kama hiyo ambayo inalenga kupunguza maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi.
“Kipekee ninawapongeza kwa ujasiri wenu wale ambao wamekuwa wakijotokeza kupima na kukutwa na maambukizi, janga hili lipo na ni letu sote, kwani naamini hakuna mtu ambaye halijamgusa kwa namna moja au nyingine hivyo niwaombe wale ambao wamegundulika na maambukizi wajitahidi kuendelea kutumia dawa za kufubaza makali ya virusi ili kuendelea kuimarika zaidi,na wale wasio na maambukizi waendelee kujilinda wao pamoja na familia zao ”Amesema Ruth.
Aidha,Bi. Ruth, amesisitiza wale ambao hawana maambukizi waendelee kuwa mabalozi wazuri kwa wengine juu ya maambukizi na wale ambao hawajatambua hali zao na wale waliotambua hali zao kuendelea kutumia dawa zakufubaza virusi na kutoacha kutumia dawa hizo kwa kuzingatia umuhimu wake.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, amewataka wenye maambukizi wasiache wala kuchoka kutumia dawa hizo kwani kwa kuzingatia umuhimu wake zina wahakikishia na zinawapa nafuu na kuondoa magonjwa nyemelezi kuendelea kuwa na afya njema na kushiriki katika shughuli za kimaendeleo na kufanya dunia mahali salama pa kuishi.
“Serikali imejipanga kuhakikisha kundi la WAVIU wote wanahudumiwa na kupatiwa mahitaji yao muhimu ikiwemo upatikanaji wa dawa za kufubaza makali ya virusi (ARV) hivyo, hivyo ni vyema sasa Serikali na wadau tukaungana pamoja kuhakikisha maambukizi mapaya ya Ukimwi yanapungua badala ya kuongezeka" Amesema Mhe. Kihanga.
Kwa upande wa Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Morogoro, Faraja Maduhu, amesema maambukizi ya Ukimwi yamepanda kwa asilimia 1.0 ambapo mwaka Julai 2021 hadi Juni 2022 watu 62,010 walipima VVU kati ya hao wanawake 4,1351 , wanaume 20,659 na waliokutwa na Ukimwi ni watu 3,527 kati yao wanaume 1,481 na wanakae 2,046 sawa na asilimia 5.6 mwaka 2021/2022 kutoka asilimia 4.6 ya mwaka 2020/2021.
Kamati ya kudhibiti Ukimwi ikiongozwa na Naibu Meya wa Manispaa ya Morogoro ambaye ni Diwani wa Kata ya Sabasaba ,akiwa na wajumbe wake waliohudhuria maadhimisho hayo pamoja na Diwani mwenyeji wa Kata ya Mlimani Mhe. Zinduna.
Post a Comment