Header Ads

DC MSULWA AZINDUA VITAMBULISHO VYA MSAMAA WA MATIBABU KWA WAZEE AWAMU YA PILI MANISPAA YA MOROGORO.

                       

                        

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa,akikata utepe kuashiria uzinduzi wa vitambulisho vya msamaha wa matibabu ya wazee.

                             

                       

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa, (watatu kutoka kulia) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Jengo la Ofisi mpya ya Ustawi.(wapili kulia) Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga , (kulia) Mganga Mkuu Manispaa ya Morogoro, Dk. Ikaji Rashid, (watatu kushoto) Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba na wawakilishi wa Wazee.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa,akigawa vitambulisho kwa Wazee.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga,akizungumza na wazee pamoja na wananchi waliojitokeza katika zoezi la uzinduzi wa vitambulisho vya msamaha wa matibabu bila malipo kwa wazee.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, akizungumza na wazee pamoja na wananchi waliojitokeza katika zoezi la uzinduzi wa vitambulisho vya msamaha wa matibabu bila malipo kwa wazee.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba,akishangilia mara baada ya kukamilika kwa uzinduzi wa Vitambulisho na Jengo la Ofisi ya Ustawi.
Afisa Ustawi Manispaa ya Morogoro, Sidna Mathias (kushoto) akisoma risala mbele ya mgeni rasmi (kulia) mratibu wa Wazee Manispaa ya Morogoro, Rehema Malimi.
Baadhi ya wazee waliohudhuria katika uzinduzi wa Vitambulisho.
                           

MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa, amezindua uzinduzi wa vitambulisho vya msamaha wa matibabu ya Wazee awamu ya pili Manispaa ya Morogoro.

Uzinduzi huo umefanyika Mei 20/2021 katika Ofisi Kuu ya Manispaa ya Morogoro ambapo ulienda sambamba na uzinduzi wa Jengo jipya la Ofisi ya Ustawi wa Jamii Manispaa ya Morogoro.

Akizungumza na Waandishi wa habari, DC Msulwa, amesema kuwa zoezi la kugawa vitambulisho kwa Wazee ni lenye manufaa makubwa kwa kundi hilo kwa vile matumizi ya vitambulisho hivyo yatasaidia moja kwa moja kutoa huduma mbalimbali ikiwemo huduma za matibabu bila malipo kwenye vituo vya afya vya Serikali.

DC Msulwa, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kutoa huduma bora zaidi kwa wazee kama inavyoelekezwa ndani ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM ya mwaka 2020-2025 na pia mpango wa pili wa Taifa wa maendeleo wa miaka mitano (2016-2021).

''Nimeambiwa kuna wazee takribani 15,631,niwapongeze sana Manispaa ya Morogoro kwa kuitikia kilio cha Wazee,tarehe 07, Mei 2021 wakati Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan alipokuwa akiongea na wazee wa Dar Es Salaam , alisisitiza suala la matibabu kwa wazee kupewa kipaumbele ikiwemo vitambulisho, na suala hili la matibau kwa wazee lililalamikiwa kuwa na changamoto nyingi, Manispaa ya Morogoro mmekuwa wa kwanza kushughulikia changamoto hiyo hongereni sana  , katika awamu hii ya pili nimeambiwa jumla ya wazee 941 kutoka Kata 13 watapatiwa vitambulisho, endeleeni na zoezi la kuwatambua wazee ili muwafikie wazee wote na hatimaye Manispaa ya Morogoro iwe ya kwanza Kitaifa kuwatambua wazee na kuwapa vitambulisho" Amesema DC Msulwa.

Aidha, ametoa rai kwa kata zoet 16 ambazo hazijakamilisha zoezi la kuwatambua wazee ndani ya Manispaa ya Morogoro zikamilishe zoezi hilo mara moja na wazee watakao tambuliwa waunganishwe  na mpango wa TASAF wa kunusuru Kaya masikini.

Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, amesema kuwa kupatiwa kadi za matibabu  kutamsaidia mzee kupata huduma za matibabu , vipimo na dawa bila malipo jambo ambalo ni msaada mkubwa kwake kwani mara nyingi umri mkubwa unaendana na kuongezeka kwa magonjwa mbalimbali hasa yale yasiyoambukiza kama vile kisukari , shinikizo la damu n.k.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, ameziomba jamii zinazoishi na wazee kuendelea kuwatunza na kuwapatia huduma nzuri ili nao wajisikie wapo katika maisha ya kujaliwa na wanamchango mkubwa katika jamii.

Lukuba,amewataka  watumishi wa kitengo cha Ustawi kuwa kilio chao cha Ofisi kimekamilika walichabakia ni kuendelea  kuchapa kazi ili jamii ziwe katika usawa unaotakiwa na kuleta maendeleo yenye usawa kwa Manispaa ya Morogoro pamoja na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wa Afisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Morogoro, Sidna Mathias,amesema kuwa Manispaa ya Morogoro imeitika agizo la kuwatambua wazee kama ilivyo kwa makundi  mengine muhimu ambapo hadi sasa jumla ya wazee 941 wametambuliwa kwa kata 13 na wazee 186 wameshatengenezewa vitambulisho huku zoezi hilo likitarajiwa kuwafikia wazee wote watakaotambuliwa wa Kata 29.

Amesema kuwa Manispaa imetenga kiasi cha shilingi milioni 10 kwa ajili ya kutekeleza shughuli za kutengeneza vitambulisho kwa Wazee wasio na uwezo.

Sidna, amesema kuwa hadi sasa jumla ya mabaraza 294 ngazi ya Mitaa yameundwa  ambapo mabaraza 29 ngazi ya Kata yameundwa katika Kata zote pamoja na baraza moja la Wilaya liloundwa jambo ambalo limepelekea Manispaa ya Morogoro kufikia asilimi 100 ya uundwaji na usimamizi wa mabaraza.

"Tunamshukuru Mkuu wetu wa Wilaya ya Morogoro , Mhe. Bakari Msulwa, kuja kutuzindulia vitambulisho na Jengo  letu, pia tunaushukuru Uongozi wa Manispaa ya Morogoro chini ya Mkurugenzi wa Manispaa ambaye amekuwa karibu na kitengo chetu kwa hari na mali , lakini tunalishukuru  Baraza la Madiwani la Manispaa kwa kukubali kutenga fedha hizi hatimaye leo tumekamilishazoezi letu , lakini  manispaa katika jitihada za kutumia vizuri fedha zake, iliamua kununua mashine kwa ajili ya kutengeneza vitambulisho hivi badala ya kumpa mdhabuni  kazi ambapo fedha nyingi zingepotea"Amesema Sidna.

"Mnamo Oktoba 2020 , Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro aliwawezesha jumla ya wazee 4 na maafisa ustawi 2 kushiriki katika maadhimisho ya wazee kimkoa yaliyofanyika Wilaya ya Mvomero, jambo hili lilitufariji sana na kuendelea kuwa na hali ya kuwatumikia zaidi Wazee kwani sisi pia ni wazee watarajiwa kwani kuna msemo unasema "Uzee na kuzeeka haukwepeki, "walikuwa kama wewe na wewe utakuwa kama wao, wazee ni hadhina tuwatunze " hivyo tunaomba jamii ichukulie umuhimu na uzito wa kuwatunza wazee hasa katika ngazi ya familia" Ameongeza Sidna.

Mbali na hapo, amesema pamoja na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Manispaa na Serikali kwa ujumla kwa kushirikiana na wadau katika kutoa hudma stahiki kwa wazee, bado eneo hilo linakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo upungufu wa Maafisa Ustawi wa Jamii, upatikanaji duni wa dawa kwa ajili ya magonjwa ya wazee , huduma za mkoba kwa wazee, uhaba wa wadau katika eneo la wazee ufinyu wa bajeti za masuala ya wazee, pamoja na kuchelewa kufanya utambuzi wa wazee wasio na uwezo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kukosekana kwa wadau wote muhimu ambao ni Mabaraza ya wazee, Uongozi wa Serikali za Mitaa , Kata na Wazee wenyewe.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.