Header Ads

MKURUGENZI MANISPAA YA MOROGORO AWAASA WATUMISHI KULINDA HISIA ZAO NA HISIA ZA WENGINE KUBORESHA UTENDAJI KAZI


MKURUGENZI wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amewaasa watumishi wa Manispaa ya morogoro  kulinda hisia zao na kuheshimu hisia za wengine ili kulinda amani, upendo, ushirikiano na kuongeza uwajibikaji mahali pa kazi na jamii kwa ujumla.

Lukuba,  amesema kuwa watumishi wa umma wanapaswa kuthamini kazi walizonazo kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma katika utendaji wao.

 “Sisi wote ni watumishi wa Serikali tunajenga nyumba moja, tuache fujo, tutembee pamoja kwa upendo na mshikamano katika kutimiza majukumu yetu kwa manufaa ya nchi na Serikali kwa ujumla linda  hisia zako ili zisiathiri tabia na mienendo yako na kusababisha kutenda matukio yasiyostahili mahala pa kazi na kwenye jamii inayokuzunguka”Amesema Lukuba.

Amesema  kuwa ni muhimu pia kuheshimu hisia za wengine kwa kuheshimu utu wao, kuwa wakarimu pamoja na kutambua na kusifia juhudi za wengine kwasababu kila binadamu ana njaa ya kutambuliwa na kusifiwa na wengine.

Aidha, amewataka watumishi wa Manispaa ya Morogoro kupendana, kuheshimiana na kuthaminiana kuanzia ndani ya vitengo na idara  ili kuongeza ari ya kufanya kazi na utekelezaji wa majukumu unaoridhisha.

Mwisho, ametoa rai kwa watumishi wa Manispaa ya Morogoro  kuhakikisha wanatoa mrejesho kwa wakati ili kusaidia utekelezaji wa majukumu na uendeshaji wa shughuli za Manispaa ili kuendelea kutoa huduma bora kwa Wananchi.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.