KAMATI YA FEDHA NA UTAWALA MANISPAA YA MOROGORO YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO
Wajumbe wakiondoka katika Soko la Kilakala.
Wajumbe wakikagua Soko la Kilakala.
KAMATI ya Fedha na Utawala Manispaa ya Morogoro imeridhishwa na kupongeza hatua ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Hayo yamejiri leo Mei 20/2021 wakati ikifanya ziara ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa na Manispaa ya Morogoro katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2020/2021
Wajumbe wa Kamati hiyo wakiongozwa na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye ni Naibu Meya wa Manispaa ya Morogoro na Diwani wa Kata ya Sabasaba , Mhe. Mohamed Lukwale, walijionea hatua za ujenzi wa ukarabati wa chumba cha darasa moja ambalo paa lake lilibomolewa na upepo mkali shule ya Msingi Towelo Kata ya Mlimani, vyumba vya madarasa Shule ya Sekondari Kihonda ambapo kwa kiasi kikubwa vimekamilika ambapo ujenzi huo unatekelezwa na Serikali pia nguvu za Wananchi zimechangiwa, Ujenzi wa Shule mpya ya mfano ya Ghorofa Kata ya Boma, Kituo cha afya cha Sina Kata ya Mafisa , Soko la Kilakala pamoja na Ukarabati wa Ukumbi wa Mikutano wa Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa miundombinu hiyo, Mhe. Lukwale, amesema kuwa kukamilika kwa Ujenzi wa madarasa kutasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa na hivyo kutekeleza kwa ufanisi sera ya elimu bila malipo.
Aidha, katika ziara hiyo, Kamati hiyo ilitembelea Soko la Kilakala huku Wajumbe hao wakitaka Uongozi wa Kata kuhakikisha kwamba wanasimamia kikamilifu Ujenzi wa Vizimba pamoja na ukarabati ili ukamilike kwa muda waliopewa na kuanza kutumika kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.
Diwani wa Viti Maalum , Mwanaidi Ngulungu, ameimba kamati ya fedha kuhakikisha kwamba fedha zilizobakia katika Soko hilo zinafika kwa wakati ili wananchi waanze kutumia vyema mradi wao ambao wamekuwa wakiusubiria kwa muda mrefu.
Kuhusu Ujenzi wa Zahanati ya Kata, Mjumbe wa Kamati hiyo ambaye pia ni Diwani wa Viti Maalum, Mhe. Zamoyoni Abdallah, amesema kwa ukubwa wa Zahanati hiyo na huduma zinazotarajiwa kutolewa hapo ni vyema Manispaa ikajipanga vizuri ili kuhakikisha wanafanya taratibu zote za kuweza kuifanya Zahanati hiyo kuwa Kituo cha afya mapema kabla ya ujenzi kukamilika.
Naye Diwani wa Kata ya Sultan Area , Mhe. Peter Dhahabu, amempongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro,pamoja na Uongozi wa Kamati ya fedha bila kumsahau Mhe. Diwani wa Kata ya Mafisa, Mhe. Joely Kisome kwa jitihada za kusimia vizuri ujenzi huo ambao unakila dalili za kukamilika na kuwahudumia wananchi.
Kwa upande wa Diwani wa Kata ya Mwembesongo, Mhe. Ally Kalungwana, amempongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro kwa ubunifu wake wa kuupendezesha Ukumbi wa Mikutano wa Manispaa huku akisema ameonesha kwamba kumbi za zamani zikisimamiwa vizuri zinaweza kuwa kumbi za kisasa kama ilivyo ukumbi huo kwa sasa.
Mhe. Kalungwana, amepongeza jitihada zote zinazofanywa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro katika kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kushirikiana na Kamati ya fedha, watumishi wa Manispaa , Wakuu wa Idara na Vitengo , wadau pamoja na Wananchi wote .
Post a Comment