Header Ads

DC MSULWA AHIMIZA WANANCHI KUDUMISHA AMANI NA UPENDO


Mkuu wa Wilaya ya Morogoro , Mhe. Bakari Msulwa, akizungumza wakati wa Iftari .
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, akizungumza wakati wa Iftari.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Morogoro Mjini, Fikiri Juma , akizungumza wakati wa Iftari.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Bakari Msulwa (wapili kutoka kulia) akikata Keki.

MKUU wa Wilya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa,  amewataka Wananchi hususani wa Wilaya ya Morogoro, kuendelea kudumisha upendo, umoja na mshikamano ikiwemo kufanya kazi kwa bidii.

Kauli hiyo ameitoa Mei 7/2021 katika Ukumbi wa Mikutano wa Manispaa ya Morogoro uliopo Soko Kuu la Chifu Kingalu wakati wa hafla fupi ya kufuturisha wananchi pamoja na waumini wa Kiislamu .

Akizungumza na Wananchi hao waliojitokeza katika iftari hiyo, DC M sulwa, amewataka wananchi kudumisha amani na upendo huku akiwasititiza kuachana na tabia ya ubaguzi. 


DC Msulwa, amewapongeza Wananchi wote waliojitokeza katika iftari hiyo aliyoiandaa , huku akiahidi  kuwa serikali itaendelea kushirikiana na Dini zote katika kudumisha amani na upendo na kuwaletea wananchi maendeleo. 

Hata hivyo, DC Msulwa, ametoa  wito kwa viongozi wa vyama vya siasa, dini na wanachi kwa ujumla kudumisha amani na utulivu uliopo bila kujali tofauti za itikadi zao, dini au makabila yao. 

“mashujaa wetu wakati wakiipigania amani ya nchi yetu hawakuangalia vyama vyao, wala dini zao, walichojali ni utanzania wao na ndiyo amani tunayojivua hadi hii leo, hivyo naomba amani tuliyonayo Watanzania tusiitie doa, tuendelee kuing'arisha kwa upendo wetu na mshikamano wetu "Amesema DC Msulwa.

Pia ametaka kuwe na vyombo vya kuleta matumaini kwenye jamii badala ya kukatishana tamaa na kukimbilia mambo yanayoashiria uvunjifu wa amani. 

Aidha, DC Msulwa,  ametuma salamu ya heri ya Sikuuu ya Eid kwa  wananchi wote na waumini wa Kiislamu wa Wilaya ya Morogoro, huku akiwaomba  waendelee kufuata misingi ya dini na kudumisha upendo katika  kuendelea kuiweka Wilaya ya Morogoro katika taswira nzuri pamoja na kuleta  maendeleo na ustawi kwa taifa.

Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro na Diwani wa Kata ya Mazimbu , Mhe. Pascal Kihanga, amewahakikishia wananchi wa Manispaa ya Morogoro  kuwa atasimamia kwa nguvu zote masuala yote yanayohusu maendeleo ya Manispaa ya Morogoro ikiwemo kudumisha mshikamano , upendo na  amani kwa faida ya wananchi wote wa Manispaa ya Morogoro. 

Mhe. Kihanga, amesema kuwa sehemu ambayo hakuna amani basi hata utulivu wa maendeleo unakosekana.

Aidha, amesema kuwa amefurahishwa sana na mshikamano wa Madiwani wake kwa kuwa na dhamira ya pamoja ya kujadiliana mambo yenye maslahi mapana ya Manispaa ya Morogoro kwa kusimamia kikamilifu Ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM ya mwaka 2020-2025.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Morogoro Mjini, Fikiri Juma, amewataka Wananchi wa Wilaya ya Morogoro kuendelea kuombea amani ya nchi bila kujali itikadi zao za vyama. 

Fikiri, amezitaka Taasisi zote zinazotoa huduma ziendelee kutoa huduma kwa kuzingatia  misingi ya sheria huku akisema kufanya hivyo ni uchamungu tosha wa kuwatumikia wananchi wao.

Akitoa mawaidha kwa Wananchi na waumini waliohudhuria katika iftari hiyo, Kaimu Shekhe wa Wilaya ya Morogoro, Mohamed Masenga ,amesema imefika mahali waislamu waondoe haya na kuwakemea wale wote wanaotaka kuvuruga amani kwa kisingizia cha dini.

Akinukuu hadithi za Mtume ,amesema kuwa Mtume Mohamad (S.a.w), aliamrisha watu wa Umma wake kuwatendea wema na kuwasamehe wale wanaowakosea badala ya kulipiza kisasi na kuhimiza kuwa Waislamu kote nchini hawana budi kufuata mafundisho hayo kwani ndiyo msingi wa maisha ya kila siku ya mwanadamu.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.