KAMATI ZA KUDHIBITI UKIMWI NGAZI ZA KATA ZATAKIWA KUTIMIZA WAJIBU YA KUZUIA MAAMBUKIZI MAPYA YA VVU.
KAMATI ya Kudhibiti Ukimwi Manispaa ya Morogoro, imezitaka Kamati za kudhibiti Ukimwi ngazi za Kata kuhakikisha zinaendelea kufanya shughuli zake na kutimiza wajibu wake kwa malengo ya kuzuia maambukizi mapya ya VVU.
Hayo yamezungumzwa Januari 28-2025 katika ziara ya Kamati hiyo inayoongozwa na Diwani wa Kata ya Mkundi na Naibu Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Seif Chomkka.
“Kama tunania ya dhati katika kupambana na maambukizi ya virusi vya Ukimwi, tuhakikishe kamati zetu ngazi za Kata zinaendelea kutimiza wajibu wake vizuri, na inayafikia makundi yote muhimu ya watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi” Amesema Mh. Chomoka.
Aidha, Mhe. Chomoka, ametoa rai kwa wadau wa maendeleo kuendelea kuyafikia makundi mbalimbali na kutoa elimu ya kutosha kwa Wananchi wote ili watu waweze kupima virusi vya Ukimwi kwa hiari na kufahamu hali ya afya zao.
Mhe. Chomoka amesema Kamati ya kudhibiti Ukimwi Kata ya Mkundi bado ni changa lakini itahakikisha wanatimiza wajibu kuendana na kasi ya kutoa elimu kwa jamii katika kutokomeza maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.
Pamoja na mambo mengine, Mhe, Chomoka , amehimiza swala la usambazaji wa zana za kujinga dhidi ya maambikizi ya VVU katika maeneo yote hatarishi ambayo kuna mikusanyiko mikubwa ya watu ili kuepukana na vitendo vya ngono zembe vinavyoweza kuongeza idadi ya maambikizi mapya.
Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro na Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Morogoro, Faraja Maduhu, amesema jamii imeendelea kuongeza kiwango cha uelewa na hivyo tahadhari zinaendelea kuchukuliwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo Wananchi kujitokeza kwa wingi kupima Afya na kupata Ushauri wa Daktari.
Post a Comment