WAZAZI, WALEZI WANAPASWA KUWAJIBIKA KATIKA MALEZI YA WATOTO.
MKURUGENZI wa Manispaa ya Morogoro, Emmanuel Mkongo, amewataka wazazi na walezi kutimiza wajibu wao wa kuwalea watoto katika misingi iliyo bora na sahihi ili kuepukana na mmomonyoko wa maadili katika jamii.
Mkongo, ametoa wito huo Desemba 31-2024 wakati wa kugawa zawadi ya Sikukuu ya Christimas na Mwaka Mpya katika Makao ya kulelea watoto ya Dar Ul Musleem Orphanage na Mgolole akiwasilisha zawadi za Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Morogoro ,Mhe. Mussa Kilakala.
Aidha,Mkongo, amesema wazazi na walezi wanajukumu la kuhakikisha wanatoa malezi yaliyo bora kwa watoto ili waweze kutimiza ndoto zao.
"Ni jukumu la kila mzazi na kila mlezi kuwa ni sehemu ya kuwajibika katika kuhakikisha kwamba watoto wanapata malezi yanayo waelekeza kuandaa kesho yao ambayo ni bora zaidi, hawa watoto ambao wanalelewa katika makao haya asilimia kubwa ni wazazi kutotimiza wajibu wa malezi na wengine kukimbia majukumu yao kama wazazi japo wapo ambao wazazi wao wameshatangulia mbele za haki na hakuna anayewajibika kuwalea "Amesema Mkongo.
Kwa upande wa Afisa Ustawi Manispaa ya Morogoro,Sidina Mathias,amewataka wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wao ili kutambua mienendo yao ambayo inaweza kusababisha kufanyiwa vitendo vya ukatili.
"Sote tunatambua kuwa watoto wamekuwa wahanga wakubwa wa vitendo vya ukatili wa kijinsia. Njia pekee ya kuwasaidia watoto ni kuwa karibu yao na ili waweze kuwaeleza viashiria vya ukatili wa kijinsia wanavyokabiliana navyo mapema kabla hali haijawa mbaya. Ukatili wa kijinsia kwa watoto unawaathiri kimwili, kihisia na kisaikolojia. Baadhi ya watoto wamepoteza ndoto katika maisha yao kutokana na vitendo hivi” Amesema Sidina.
.
Post a Comment