DC KILAKALA AKABIDHI HUNDI YA MILLIONI 699 NA KUGAWA VITAMBULISHO VYA WAMACHINGA
MKUU wa Wilaya ya Morogoro , Mhe. Mussa Kilakala, amekabidhi hundi ya jumla ya kiasi cha Tshs 699,411,000/= kwa ajili ya utoaji wa mikopo kwa makundi ya Vijana, Wanawake na Watu wenye Ulemavu katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro sanjari na kugawa vitambulisho vya wajasiriamali wadogowadogo (Machinga).
Zoezi hilo limefanyika Ukumbi wa Kilakala Soko Kuu la Chifu Kingalu.
" Mikopo hii ilisimama kutokana na kuibuka tabia ya vikundi kubadili matumizi ya fedha za mikopo na wengine kukimbia na fedha hizo lakini kuwanufaisha watu ambao sio walengwa wa mikopo,tunamshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kurejesha fedha hizi kwenye mfumo mzuri na uliobora ,rai yangu tumieni fedha hizi kwa malengo yaliyokusudiwa sio kwenda kuzichezea ngoma na sherehe, watakaoenda kinyume tutawachukulia hatua kali za kisheria " Amesema DC Kilakala.
DC Kilakala,amesema Dkt.Samia lengo lake ni kuona watu wachini wanajikwamua kiuchumi na kuboresha maisha yao, hivyo amewataka wanavikundi kutorudia makosa yaliyopelekea kusitishwa kwa mikopo hiyo.
Pia,amesema wanawake wamekuwa mfano wa kuigwa katika urejeshaji wa mikopo,amewaomba wakae na Vijana ambao ni watoto wao wawasisitizie juu ya urejeshwaji wa mikopo na watimize malengo ya fedha hizo za mkopo ili wengine waweze kukopeshwa.
Aidha,amewataka viongozi wa Serikali hususani wataalamu wa idara ya mikopo,watumie muda mwingi kuwaelimisha wananchi juu ya vigezo vya kupata mikopo na pale wanapokosea wawasahihishe badala ya kuwarudisha nyumbani.
Hata hivyo, amezitaka kamati za Mikopo kutoa elimu kwa vikundi ambavyo havijakidhi vigezo vya kupata mkopo kwa sasa ili wanakikundi wakamilishe taratibu zote zinazotakiwa kwaajili ya kupata mkopo kwa wakati mwingine.
Katika hatua nyengine,amewahimiza wazazi juu ya malezi ya watoto kutokana na wimbi la ukatili watenge muda wa kukaa na watoto wao badala ya kujikita zaidi kwenye utafutaji wa fedha.
Naye , Kaimu Mwenyekiti Kamati ya Mikopo ya Wilaya, Hilary Sagara,amesema jumla ya vikundi 55 wamepewa mkopo huo ikiwa vikundi vya Wanawake ni 33, Vikundi vya Vijana ni 15 na Vikundi vya watu wenye Ulemavu ni 07
Kwa upande wa Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, amezitaka kamati za mikopo kuwa wazi kuielezea jamii taratibu zinazotakiwa kwa vikundi vinavyopaswa kupata mikopo ili kuondoa malalamiko kwa wale watakaokosa mkopo kutokana na kushindwa kuwa na sifa zinazotakiwa.
Akizungumza kwa niaba ya wanavikundi , Nasibu Said, ametoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii, kwa kuwawezesha kupata mkopo utakaotumika kuboresha maisha yao.
Nasibu amesema , watahakikisha wanaendelea kutoa ushirikiano na kuwa waaminifu katika kurejesha mikopo yao ili kuendeleza zoezi hili kwa wote wenye sifa za kupokea mkopo huo.
Post a Comment