Header Ads

SUALA LA UPATIKANAJI WA CHAKULA MASHULENI IWE NI SHIRIKISHI ZAIDI-SAGARA



KAIMU Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Hilary Sagara, amesema suala la utoaji lishe shuleni liwe shirikishi katika   jamii kwa kila mmoja kushiriki kwa kuhakikisha inakuwa ni ajenda ya kudumu kwa lengo la kuimarisha na kujenga afya za wanafunzi ili waweze kupata chakula pindi wawapo shuleni jambo litakalosaidia wanafunzi kupata elimu kwa kuzingatia masomo yao vizuri.

Hayo ameyasema katika Kikao  cha Tathmini ya Lishe kilichofanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya Morogoro Ofisi Kuu Agosti 16-2024.

Sagara, amesema kuwa suala la lishe ni shirikishi kwa jamii nzima kwani upatikanaji wa chakula hutegemea na aina ya chakula kinachopatikana katika maeneo husika, hivyo si lazima chakula kiwe ni mahindi na maharage bali ukusanyaji wa vyakula uzingatie nyakati na upatikanaji wake katika maeneo husika.

Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga,  amesisitiza watendaji wa kata kushirikiana kwa ukaribu na jamii husika na uongozi wa Mitaa  kwa kuwa na vikao vya pamoja ili kupata suluhu ya upatikanaji wa chakula shuleni kwa watoto wote ikiwemo kutumia mbinu mbalimbali za ushawishi  ili kutekeleza agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la upatikanaji wa chakula  shuleni  na kwamba kwa agizo hili kila mtendaji atapimwa namna anavyotekeleza agizo hili.

Naye Katibu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Morogoro Mjini, Twalib Bellege,  ameyataka Mabaraza ya  Maendeleo ya kata(BMK) kufanya ajenda ya  upatikanaji wa chakula kuwa ajenda muhimu na shirikishi ikiwemo upangaji wa bajeti ya chakula shuleni, huku upande wa ugonjwa wa kipindupindu ametaka kuendelea kutolewa kwa elimu ya afya na usafi wa mazingira inazingatiwa kwa kuzingatia matumizi ya maji safi, uimarishaji wa miundombinu ya maji na matumizi ya vyoo bora na salama.


Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Christopher Komba,  amesema kuwa watendaji wa kata wamepewa dhamana ya kuongoza katika maeneo yao hivyo wanalo jukumu la kusimamia utekelezaji wa agizo la upatikanaji wa chakula mashuleni ni vema wakazingatia zaidi mazingira ya maeneo yao ili kuleta matokeo mazuri kwa kuzingatia zaidi matumizi ya njia shirikishi kwa jamii kwa jamii husika kushiriki kwa ukubwa zaidi kutoa mawazo yao kupitia mikutano ya Mitaa  na kamati za shule jambo litakaloleta tija kwa wanafunzi .


Mkuu wa Divisheni ya Afya Dkt..Maneno Focus,  amesema Divisheni ya Afya inaendelea kusimamia suala la lishe na utekelezaji wa agizo la Rais lakini pia inaendelea kutoa  elimu ya usafi wa afya na mazingira katika maeneo mbalimbali huku akitoa rai kwa watendaji kuendelea kuhamasisha suala la usafi wa mazingira kwa wananchi katika maeneo mbalimbali ikiwemo majumbani na maeneo ya biashara ili kujiepusha na magonjwa ya mlipuko ikiwemo ugonjwa wa kipindupindu.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.