WADAU WA AFYA WATAKIWA KUENDELEZA MAPAMBANO DHIDI YA USUGU WA VIMELEA VYA DAWA.
WADAU wa afya wametakiwa kuendeleza mapambano dhidi ya tatizo la usugu wa vimelea vya dawa kwa kuongeza uelewa kwenye jamii na kutia hamasa kuhusu usugu wa dawa za binadamu ambao unatishia afya za binadamu duniani kote.
Hayo yamelezwa leo Machi 29/2022 na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dr.Kusirye Ukio, akimwakilisha Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro katika Semina ya mafunzo ya matumizi sahihi ya dawa zenye asili ya kulevya (Controled drugs) yaliyofanyika katika Ukumbi mdogo wa Makataba ya Mkoa wa Morogoro iliyopo Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza na Wafamasia walioshiriki katika Halamashauri zote Mkoa wa Morogoro , Dr Ukio, amesema licha ya juhudi za serikali katika kuhakikisha wananchi wake wanakuwa na afya njema bado kuna jitihada binafsi ambazo zinatakiwa kufuatwa zinazozingatia i taratibu za kitabibu katika kutibu wagonjwa kwa kuwapatia dawa kwa utaratibu maalumu.
" Kuna umuhimu wa elimu zaidi kutolewa kwa jamii ili kuongeza uelewa kuhusu usugu wa dawa za binadamu unaotokana na utolewaji wa dawa kiholela bila cheti cha daktari na kusababisha madhara kwa afya ya binadamu, hivyo nitoe ushauri kwa wadau wa afya hususani wafamasia kuwa na utaratibu wa kutoa huduma baada ya kupokea cheti kutoka kwa Daktari ili kunusuru afya za wateja wetu" Amesema Dr. Ukio.
Dr. Ukio, amesema zipo sababu zinazochangia usugu wa dawa kwa binadamu kuwa ni pamoja na kutumia dawa bila kupima na kupata ushauri wa kitabibu,kutokukamilisha dozi pamoja na matumizi ya dawa za binadamu kwa mifugo .
Naye Meneja wa TMDA Kanda ya kati zikijumuisha mikoa ya Morogoro, Singida, Dodoma na Iringa, Bi. Sonia Mkumbwa, amewataka Wafamasia kujenga utaratibu wa kupitia mara kwa mara katika maduka na vituo vyao vya afya kupitia na kuona matumizi ya dawa hizo yanavyotumika kama yanazingatia taratibu au la.
Bi. Mkumbwa, amesema kuwa Usugu wa dawa ni hali ya dawa kushindwa kuua vimelea vya magonjwa au kuzuia ukuaji wake na hivyo dawa kushindwa kudhibiti vimelea hivyo.
" Mafunzo haya muhimu sana kwenu, tunaendelea kukumbushana ili tuzingatie sheria na miongozi ya matumizi ya dawa hizi kwa wafamasia wetu, lakini nipende kuiambia jamii kuwa vimelea vya magonjwa ndio hujenga usugu wa dawa , jamii inapaswa kupiga vita matumizi mabaya ya dawa, lazima tuwe na huruma kwa binadamu wenzetu,ikiwa sheria na miongozo ya kiafya itafuatwa itasaidia wafamasia kufanya kazi kwa weledi ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa sheria za afya”Amesema Bi. Mkumbwa.
Kwa upande wa Mfamasia wa Mkoa wa Morogoro, Bi. Neema Shanalingigwa, amefurahishwa na mafunzo hayo ya matumizi sahihi ya dawa zenye asili ya kulevya, huku akiwataka Wafamasia wote Mkoa wa Morogoro kuhakikisha wanasiamamia vyema suala la utoaji wa dawa hizo na kupitia mara kwa mara katika maduka yote ya dawa ambayo yanatoa huduma za dawa.
Katika hatua nyengine, miongoni mwa Wafamasia akiwemo Mfamasia wa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, Joyceline Boniphace, ameseam atahakikisha kwamba mafunzo hayo yanazaa matunda kwani watajipanga kikamilifu kuona dawa zote zikiwemo dawa zenye asili ya kulevya (Controled drugs) ikiwamo Narcotics na Psychotropics zinafuata utartibu katika matumizi yake.
Post a Comment