Header Ads

TAS YATAKA WATU WENYE ULEMAVU WASITENGWE.

Mwenyekiti wa TAS, Hassan Mikazi, akimkabidhi cheti cha kushiriki mwandishi wa habari kutoka redio Okoa FM.
Waandishi wa habari wakifuatilia kwa makini mafunzo.

CHAMA Cha watu wenye ualbino Mkoa wa Morogoro (TAS), kimetoa wito kwa Serikali na taasisi  za kiraia kuboresha mifumo ya ajira na miundombinu isiyo na ubaguzi kwa watu wenye ulemavu.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa TAS , Hassan Mikazi,  katika mkutano na wanahabari Mkoa wa Morogoro katika Ofisi yake iliyopo Kilakala Manispaa ya Morogoro Machi 26/2022 wakati wa mafunzo ya mradi wa ajira jumuishi kwa watu wenye ulemavu.

“Serikali itoe elimu inayohusisha kutengeneza sera na miongozo, vipeperushi na mabango kwa ajili ya kuelimisha jamii kwamba watu wenye ulemevu wanaweza kufanya kazi kama watu wengine, tunasisitiza hili kwa sababu watu wenye ulemavu wanapokwenda kuomba kazi kwenye taasisi mbalimbali hawapati mapokezi mazuri, yaani wanaonekana kama ni watu ambao hawawezi kufanya kazi yoyote ile" Amesema Mikazi.

“Tunapaswa kuwajumuisha watu wenye ulemavu katika shughuli zetu, kwa sababu wana talanta ambayo wamepewa, wana vitu vya ziada ambavyo wamepewa na Mwenyezi Mungu, jamii  ielimishwe kuwatambua watu wenye ulemavu kwamba wana uelewa kama watu wengine na ni watu ambao wana juhudi kubwa katika kufanya kazi,”Ameongeza Mikazi.

Kwa mujibu wa Mikazi, utafiti walioufanya TAS katika maeneo tofauti tofauti, ubebaini kuwa watu wengi hawaamini kwamba watu wenye ulemavu wanaweza kufanya kazi kama watu wengine katika jamii.

Mikazi, amesema miundombinu iliyo rafiki kwa watu wenye ulemavu pia ni changamoto kubwa katika ofisi nyingi za Serikali na taasisi za kiraia. ambapo hata Ofisi nyingi zina ngazi ndefu zisizo rafiki kwa watu wenye walemavu.

Pia, amesema utafiti umebaini kuwa baadhi ya watu wamejenga dhana kwamba mlemavu akionekana kwenye ofisi fulani anakuwa amekwenda kuomba msaada, kumbe wakati mwingine amekwenda kufuatilia haki zake mbalimbali.

Hata hivyo, Mikazi ,amesema wamegundua  kwamba hata kwenye suala la mikopo, watu wenye ulemavu hawajaangaliwa sana, ingawa nao wanastahili kupewa mikopo kupitia asilimia mbili kati ya 10 inayotolewa kwenye halmashauri kutokana na mapato ya ndani.

Mikazi, amesema wanaendelea kutoa elimu ya kuhamasisha makundi ya rika, jinsi na hali zote kuwathamini watu wenye ulemavu na kuwashirikisha katika shughuli mbalimbali ambapo kwa sasa wameanza na Waandishi wa habari, na kufuatia walengwa pamoja na waajiri.

Mwisho, Mikazi,  amefafanua kuwa wanatumia mikutano mbalimbali kama vile semina na makangamano kueneza elimu hiyo kupitia mradi wa ajira jumuishi kwa watu wenye ulemavu, chini ya ufadhili wa Shirika la INTERNEWS.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.