JAFO AWATAKA TFS KUANZISHA VITALU MASHULENI.
Mkuu wa Wilaya ya Gairo Jabiri Makame akitoa taarifa kuhusu Kampeni ‘Urithi wa Kijani Gairo’ katika viwanja vya Shule ya Sekondari Gairo wilayani humo mkoani Morogoro Machi 30, 2022.
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akizindua Kampeni ‘Urithi wa Kijani Gairo’ katika viwanja vya Shule ya Sekondari Gairo wilayani humo mkoani Morogoro Machi 30, 2022.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela Dkt. Selemani Jafo akizungumza na wadau mbalimbali wa mazingira na wanafunzi wakati wa uzinduzi wa Kampeni ‘Urithi wa Kijani Gairo’ katika viwanja vya Shule ya Sekondari Gairo wilayani humo mkoani Morogoro Machi 30, 2022.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akishiriki na viongozi mbalimbali na mabalozi wa mazingira katika matembezi kuelekea katika viwanja vya Shule ya Sekondari Gairo kwa ajili ya uzinduzi wa Kampeni ‘Urithi wa Kijani Gairo’ Machi 30, 2022.
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ametoa wito kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuanzisha vitalu vya miche ya miti katika shule za msingi na sekondari nchini.
Ametoa wito huo wakati akizungumza Machi 30, 2022 kwenye uzinduzi wa Kampeni ya ‘Urithi wa Kijani Gairo’ inayotekelezwa na Wilaya ya Gairo mkoani Morogoro na kutoa pongezi kwa uongozi wa wilaya na mkoa kwa kuasisi kampeni hiyo.
Waziri Jafo alisema shule zikiwa na vitalu itasaidia kupata miche ya miti kwa wingi ambayo itasambazwa, kuoteshwa na kutunzwa katika halmashauri nchini hatua itakayoifanya Tanzania kuwa ya kijani kama maelekezo ya Serikali yalivyotolewa.
“Ndugu zangu wa TFS niwapongeze sana kwa kuwezesha zoezi la upandaji miti kwani nimepita maeneo mengi nimeona mmefanya kazi, niwapongeze pia mabalozi wetu wa mazingira mnajituma sana kuikijanisha nchi yetu.
Sasa niwaombe TFS hakikisheni mnazipatia miche shule za msingi na sekondari, lengo letu ni kuwa halmashauri zote 184 zikipanda miti milioni moja na nusu kila moja basi tutakuwa tumepanda miti takriban milioni 276 kila mwaka,” alisema.
Waziri Jafo alisema kuwa suala la mazingira halina mjadala ni ajenda yetu sote na ndio maana Serikali imetoa maelekezo kuhusu kila mtu au taasisi kushiriki katika utunzaji wa mazingira.
Alisema kuwa Mkoa wa Morogoro una kila sababu ya kuhakikisha mazingira yanatunzwa kwa kuwa kuna miradi mbalimbali ya kimkakati ukiwemo wa Bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere na Kidatu ambalo linahitaji maji wakati wote.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Gairo Jabiri Makame alisema kampeni hiyo mbali ya kutekeleza maelekezo ya Serikali pia inalenga kurejesha hali ya ukijani iliyokuwepo wilayani humo.
Alisema kuwa wilaya hiyo imekuwa ikikabiliwa na uharibifu wa mazingira sambamba na kuongezeja kwa joto hivyo kukawa na umuhimu wa kuwashirikisha wadau mbalimbali kuja na mkakati wa kurejesha asili yake kwa kupanda miti.
DC Makame, alisema kutokana na hamasa ya wananchi kumekuwa na uhitaji mkubwa wa miche ya miti hvyo viongozi wilayani humo wanaendelea kuhamasisha wadau kuzalisha miche kwa wingi ili kukidhi mahitaji..
Post a Comment