RC SHIGELA ATAKA ZOEZI LA ANWANI ZA MAKAZI LIZINGATIE UADILIFU.
MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Martine Shigela, amelitaka zoezi la Anwani za Makazi lizingatie uadilifu ili kuhakikisha taarifa zote zinazohitajika zinaingizwa kwenye mfumo.
Kauli hiyo ameitoa leo Machi 11/2022 katika Mafunzo
ya Anwani za Makazi na Posti kodi katika Ukumbi wa Tanzanite Manispaa ya
Morogoro.
Akizungumza na wataalamu pamoja na waendeshaji wa
zoezi hilo, RC Shigela, amesema uadilifu ni kitu kitakachopelekea zoezi hilo
kukamilika bila dosari zozote.
RC Shigela,
amesema kuwa katika utekelezaji wa zoezi
hili hakuna mbadala isipokuwa ni kutekeleza kwa nguvu zote kwani Serikali ya
Awamu ya Sita inadhamiria kuwasaidia Wananchi katika kuboresha mawasiliano katika
sehemu mbalimbali ikiwemo makazi yao, sehemu zao za biashara na maeneo mengine
ya huduma za kijamii.
RC Shigela, amesema utekelezaji wa zoezi la Anwani za Makazi ni Jambo la kihistoria ambapo Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuacha alama kwa watanzania na lengo lake ni kurahisisha mawasiliano na kuifanya jamii kuwa ya kisasa zaidi bila kusahau kuimarisha ulinzi katika makazi yao.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Morogoro, Bi, Dorothy
Mwamsiku, amewataka wale wote wenye nia ovu la kukwamisha zoezi hilo waache mara
moja.
Aidha,
Mwamsiku ,amesema hawatamchekea mtu yeyote atakaye vuruga zoezi hilo na kwamba
ikitokea kuna watu wamevuruga basi hatua kali za kisheria zitachukuliwa zidi
yao.
Mwamsiku, ameutaka Uongozi wa CCM kutoka ngazi ya mkoa mpaka ngazi ya tawi kuhamasisha jambo hilo kwani ni moja ya utekelezaji wa ilani ya chama hicho ambapo wenyewe ndiyo wasimamizi.
Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Albert Msando, amesema kuwa zoezi la uwekeji wa anwani za makazi na Postikodi litarahisisha utambuzi wa maeneo ya shughuli mbalimbali za mkoa wa Pwani yakiwemo maeneo ya viwanda.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP
Fortunatus Musilim, , amesema Jeshi la Polisi lipo makini katika kufuatilia
zoezi hilo ili kuhakikisha kwamba zoezi hilo linafanyika kwa Amani.
Musilim , amewataka wale waliopewa nafasi ya kusimamia
zoezi hilo walifanye kwa uadilifu kwa kuwa wameaminiwa na Taifa katika
kufanikisha zoezi hilo lenye malengo makubwa katika maendeleo ya Taifa
“Niwaombe wasimamizi wa zoezi hili tunataka zoezi
liwe la uadilifu na Amani, niombe sana washiriki msinipangie kazi nina kazi
nyingi za kufanya sasa sitarajii kuona zoezi hilo linavurugwa , ukiona mtu anataka
kuhatarisha Amani ya zoezi hili tunaomba sana toa taarifa mapema “ Amesema Musilim
.
Post a Comment