MANISPAA YA MOROGORO YATOA MKOPO WA SHILINGI MILIONI 631 KWA VIKUNDI MWAKA WA FEDHA 2021/2022.
HALMASHAURI ya Manispaa ya Morogoro imetoa fedha kwa ajili ya mikopo yenye jumla ya milioni 631,150,000/= kwa vikundi vya vijana 60 ikiwamo vikundi 39 vya Wanawake, vikundi 16 vya Vijana na Vikundi 5 vya Watu wenye ulemavu.
Hundi hiyo ya Mkopo yenye thamani ya Shilingi Milioni 631,150,000/=imetolewa mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Martine Shigela, Machi 08/2022 katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika katika Uwanja wa Jamhuri Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza wakati wa kukabidhi hundi hiyo kwa vikundi, RC Shigela, amewataka wanufaika wa mikopo hiyo kutumia mikopo kwa kuanzisha shughuli zitakazobadili maisha yao na kuwa bora zaidi.
Aidha, RC Shigela, amewataka wanufaika wa mkopo kurejesha mikopo hiyo kwa wakati ili kuwezesha watu wengine kukopa na kujikwamua kutoka katika hali duni ya maisha.
Hata hivyo, RC Shigela, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wananchi wake kuwa huku akisema Mhe. Rais ametoa mikopo hiyo ikiwa ni kuwezesha wananchi anaowaongoza kuondokana na hali duni ya maisha baada ya kupata mikopo na kuanzisha shughuli za uzalishaji mali.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, amewasisitiza wanufaika wote waliopatiwa mikopo kuzitumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa na kuwaagiza watendaji wa kata na maafisa Maendeleo ya jamii kusimamia vikundi na kuelewa fedha iliyotolewa ni kodi za wananchi hivyo zinapaswa zitumike na kurejeshwa ili vikundi vingine navyo viweze kukopeshwa.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Ally Machela, amesema kuwa Manispaa ya Morogoro hutenga 10% ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kukopesha vikundi vya wanawake na vijana na watu wenye mahitaji maalumu,ambapo asilimia 4 ni kwa vikundi vya wanawake na asilimia 4 ni kwa vikundi vya vijana na asilimia 2 ni kwa watu wenye ulemavu.
"Leo tumetoa hundi hii kwa vikundi vyetu kupitia mapato ya ndani, fedha hizi za mkopo ni fedha za kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 kwa ajili ya kuvikopesha vikundi vya vijana, Wanawake na Watu wenye ulemavu." Amesema Machela.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Morogoro, Enedy Mwanakatwe, amesema lengo la mfuko wa maendeleo ya wanawake na vijana na watu wenye ulemavu ni kutoa fursa kwa jamii hivyo ili waweze kupata mikopo isiyo na riba ili kuwaongezea mitaji kwenye biashara ambazo tayari zimeanzishwa katika kuwawezesha kujiendeleza kiuchumi na hivyo kuinua hali za maisha.
"Vikundi vinavyopewa mikopo ni vile ambavyo vimependekezwa na kamati za maendeleo za kata na kufanyiwa uhakiki na kuonekana vimekidhi vigezo, ombi langu mikopo hii sio misaada tumekopeshwa turejeshe kwa wakati na kuitumia katika malengo tuliyotarajia na kujiwekea kama vikundi" Amesema Mwanakatwe.
Katika mchanganuo wa mkopo wa milioni 631,150,000/=, shilingi milioni 409,000 zimetolewa kwa vikundi vya Wanawake, Shilingi milioni 186,000 zimetolewa kwa Vijana na shilingi milioni 36150 zimetolewa kwa watu wenye ulemavu.
Post a Comment