MANISPAA YA MOROGORO YAPANDA MITI ZAIDI 200 SHULE YA MSINGI TUBUYU,AFISA NEMC ATOA ONYO KWA WANAOTUMIA MIFUKO YA PLASTIKI
AFISA Mazingira Mwandamizi kutoka NEMC , Meshack Mtakia, amewataka wananchi kutafuta na kupata uelewa wa taarifa mbalimbali zinazohusu makatazo ya mifuko hiyo ili kuepuka adhabu zilizowekwa.
Kauli hiyo ameitoa Juni 04-2025 katika zoezi la upandaji wa Miti shule ya Msingi Tubuyu Kata ya Tungi lililoratibiwa na Manispaa ya Morogoro kwa kushirikiana na wadau wa Mazingira ikiwa ni kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani Juni 05-2025
Mtakia, ameonya kuwa, mtu kutojua sheria si kigezo cha kumfanya asiadhibiwe pale ambapo atapatikana na kosa la kuvunja sheria.
“Wajibu wa wananchi ni kutafuta taarifa sahihi za makatazo ya mifuko ya lastiki. Zoezi la ukaguzi linapoanza atakayekutwa na mifuko ya plastiki atapigwa faini kwa mujibu wa sheria” Amesema Mtakia
Naye Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Maliasili na Mazingira, Dauson Jeremia, amewataka wananchi kujenga tabia ya kufanya usafi katika maeneo yao mara kwa mara ili kuepuka magonjwa ya milipuko.
Dauson, amesema Manispaa katika kuadhimisha siku Mazingira Duniani ,imeshirikiana na Wadau wa mazingira kupanda miti pamoja na kufanya usafi ikiwa njia moja wapo ya kuelimisha jamii kuhusiana na masuala ya usafi kwa kupenda mazingira yaliyo safi kwa usalama kwa afya zao.
Kwa upande wa Wadau wa Mazingira kutoka Shirika la Agriwezesha , Mkurugenzi wa shirika hilo,Deograsia Chuma ,amesema kama shirika limeungana na Manispaa kuhakikisha jamii inakuwa na mazingira bora hususani katika suala zima la upandaji wa miti shuleni ambapo kwa ufadhili wao wametoa zaidi ya miti 200 eneo la shule ya Msingi Tubuyu.
Aidha, Mkurugenzi wa Shirika la Mother of Mercy , Gration Mbelwa, amesema wameshirikiana na Manispaa ikiwa ni muendelezo wao wa kuhamasisha jamii juu ya masuala mazima ya upandaji wa miti lakini na kuhamasisha wananchi juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti wa Shirika la Morogoro Waste For Value, Omary Jumanne, amesema shirika lao limekuwa likijihusisha na uchakataji wa taka za plastiki ambapo lengo ni kupunguza taka za plastiki mitaani lakini kuonesha fursa na thamani ya taka za plastiki.
Naye Balozi wa Mazingira na uhifadhi wa vyanzo vya Maji, Msanii nguli hapa nchini, Afande Sele,amesema ataendelea na jitihada zake za kuelimisha jamii juu ya masuala ya mazingira pamoja na uhifadhi wa vyanzo vya maji.
Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani litafanyika Juni 05-2025 katika Ukumbi wa Manispaa ya Morogoro.
Post a Comment