DC KILAKALA AWATAKA WANANCHI KUFUCHUA WAHARIFU WA VITENDO VYA UKATILI DHIDI YA WATOTO
MKUU wa Wilaya ya Morogoro Mhe.Mussa Kilakala,amewataka
wananchi kuwafichua wanaotenda makosa ya ukatili dhidi ya Watoto katika Jamii.
Kauli hiyo ameitoa Juni 16-2025 katika maadhimisho ya Siku
ya Mtoto wa Afrika Manispaa ya Morogoro iliyofanyika eneo la Uwanja wa Mpira wa
Miguu Shule ya Msingi Mwembesongo.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza katika maadhimisho
hayo,DC Kilakala,amesema siku ya Mtoto wa Afrika ni vyema jamii ikafanya tathimini
ya hali halisi iliyopo kwa kutafakari Kauli mbiu ya Siku ya Mtoto wa Afrika
mwaka 2025 inayokumbusha kuangalia mienendo dkatika makuzi na malezi ya Watoto wakiwa
nyumbani, nje ya nyumbani kwa kuangalia walipotoka,walipo na wanapoenda na
kurekebisha mapungufu ili kuangalia kesho yao kwa malezi bora.
ameiomba Jamii kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi
kuhakikisha vitendo vya ukatili dhidi ya Watoto vinakemewa vikali na kuzuiwa
katika Jamii.
DC Kilakala, amewataka wazazi/walezi na wadau wa masuala ya Watoto kwa kila mmoja
aone kwamba ana wajibu wa kuleta mabadiliko chanya kwa jamii kushiriki
kikamilifu katika kulinda na kutekeleza kwa vitendo Haki za Watoto.
“Tuna wajibu wa kutoa elimu kwa Watoto wetu juu ya
mabadiliko mbalimbali ya kijamii ikiwemo matumizi ya teknolojia ambapo ukuaji
wake uendane na ukuaji wa elimu ili matumizi yake yasiwe na athari hasi katika
maendeleo ya ukuaji na hatma ya Maisha ya watoto wetu” Amesema DC Kilakala.
Mwisho,ameitaka Jamii kukabiliana na mmomonyoko wa maadili
kwa kukemea hali ya ukiukwaji wa maadili mema hususani katika kuingiza
mila,desturi na tamaduni zisizokubalika na kulinda mila na desturi nzuri kwa Watoto na jamii kwa
ujumla.
Naye Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii Manispaa ya
Morogoro,Faraja Maduhu,amesema siku hii huadhimishwa kwa lengo la kutambua
thamani,utu na umuhimu wa Mtoto Duniani kutokana na mauaji ya Watoto takribani
2000 yaliyofanywa na utawala wa Makaburu katika Kitongoji cha Soweto Nchini
Afrika Kusini tarehe 16,Juni mwaka 1976.
Maduhu amesema Kauli Mbiu yam waka 2025 inaitaka Jamii
kutafakari upatikanaji wa haki haki za Watoto tangu zilipoanzishwa na Sera ya
Maendeleo ya Mtoto yam waka 2008 ambayo inakumbusha wazazi au walezi na jamii
haki tano za msingi za mtoto ikiwemo kuishi, kulindwa, kuendelezwa,kutobaguliwa
na haki ya kushiriki na kutoa maoni kwa mambo yanayomuhusu.
Kwa upande wa Mratibu wa Dawati la Maendeleo ya Mtoto
Manispaa ya Morogoro,Joyce Mugambi,amesema elimu za kupinga ukatili ulitolewa
kwa Kata 12 na kufikia shule za Msingi 14 na vituo vya kulelea Watoto 4 ,kutoa
elimu Kamati za usalama shuleni kwa Zaidi ya shule za Msingi 128,kuhuisha Mabaraza
ya Kata 23 na Mitaa 135 ,kutoa elimu juu ya haki na wajibu ambapo jumla ya
shule 17 za Msingi na wanafunzi Zaidi ya 658 wamefikiwa na elimu hiyo.
Kauli Mbiu ya Siku ya Mtoto wa Afrika mwaka 2025 inasema “Haki za Mtoto:Tulipotoka,Tulipo na Tuendako”.
Post a Comment