Header Ads

DC WAKUU WA SHULE , WENYEVITI WA BODI NA MAAFISA ELIMU KATA WATAKIWA KUINUA UFAULU SHULENI



WAKUU  wa Shule za Sekondari ,Wenyeviti wa Bodi pamoja na Maafisa Elimu Kata Manispaa ya Morogoro  wametakiwa kusimamia elimu ili kufikia malengo ikiwa ni pamoja na kukuza ufaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza, la pili na la tatu lakini pia kupunguza kiwango cha wanafunzi wanaofeli.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro,Mhe. Mussa Kilakala,  wakati akizungumza na wakuu wa shule za sekondari, Wenyeviti wa bodi pamoja na Maafisa Elimu Kata katika kikao kazi cha Tathmini ya matokeo ya Kitaifa ya mwaka 2024 kwa Shule za Sekondari katika Ukumbi wa Bwalo Shule ya Sekondari Kilakala.

Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga , amesema kuwa  malengo ya Halmashauri katika upimaji wa kidato cha pili na kidato cha nne kwa mwaka 2025 ni kufuta daraja sifuri na kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi anayemaliza kidato cha nne anapata cheti lakini pia kupunguza ufaulu wa daraja la nne na kuongeza ufaulu bora yaani daraja I, II, na III.

Akiwasilisha taarifa ya matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha pili na kidato cha nne kwa mwaka 2024, Mkuu wa Divisheni ya Elimu Sekondari, Sylevestr Mwenekitete, amesema kuwa  matokeo sio mabaya kwa  kwa  wanafunzi wa kidato cha pili waliopimwa na kidato cha nne  hivyo ameomba jitihada za makusudi ziongezwe ili Manispaa katika matokeo ya mwaka 2025 iwe ya Kwanza Kimkoa na Kitaifa.

Katika hatua nyingine, Mwenekitete, amewapongeza wakuu wa shule ambao shule zao zimefanya vizuri na kuwataka kuziendeleza jitihada hizo huku akiwataka wakuu wa shule ambazo hazikufanya vizuri kuongeza jitihada ili wapate matokeo mazuri katika mitihani inayofuata.

Naye mwakilishi wa Afisa Elimu Mkoa wa Morogoro, Bi. Hildegard Saganda,  amewataka wakuu wa shule pamoja na Maafisa Elimu Kata kusimamia nidhamu shuleni ikiwa ni pamoja na kuzuia utoro wa wanafunzi pamoja na walimu ili kuinua taaluma kwani vitendo hivyo huathiri tendo la ufundishaji na ujifunzaji.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.