KAMATI YA CHAKULA NA VIPODOZI YATAKIWA KUJIKITA KATIKA UTOAJI WA ELIMU KWA WAFANYABIASHARA
KAMATI ya Chakula na Vipodozi Manispaa ya Morogoro imetakiwa kujikita katika kuoa elimu kwa wafanyabiashara ili kuwatengenezea wafanyabiashara mazingira mazuri ya biashara zao kwa wateja.
Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye ndiye Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro,Emmanuel Mkongo wakati akizindua rasmi kamati hiyo Juni 27-2025.
Mkongo,amesema elimu iwe kipaumbele kwa kamati,kuliko kuchukua hatua kwani wakichukua hatua zaidi bila elimu italeta taharuki kwa wafanyabiashara.
"Leo tumezindua kamati hii,niombe ushirikiano kwenu wajumbe,tukafanya kazi kwa uaminifu na kuepusha malalamiko, kikubwa mkajikite kutoa elimu, ikiwezekana kabla ya kwenda kukagua muwasiliane na wafanyabiashara kwa maandiko ili ikitokea changamoto tujue njia ya kuitatua " Amesema Mkongo.
Hata hivyo,amesema kuwa kamati hiyo itakuwa na majukumu ya Kujadili na kuidhinisha maombi ya vibali,Kupokea na Kujadili taarifa za ukaguzi na ufuatiliaji na Kuainisha shughuli za udhibiti wa vyakula, na vipodozi kama kipaumbele kinachotakiwa kuingizwa kwenye mwongozo wa bajeti.
Pia ,amesema kamati hiyo itakuwa inakaa vikao vyake vya kisheria kila baada ya robo ili kutathimini utendaji kazi wa kamati hiyo.
Aidha, Mkongo,amewataka wenye maduka ya dawa na vyakula kuhakikisha wanakagua mara kwa mara bidhaa zao ili kuhakikisha wanauza bidhaa ambazo hazijakwisha muda wa matumizi lakini pia wahifadhi vizuri bidhaa zao sehemu ambazo ni safi na salama
Naye Afisa Afya Manispaa ya Morogoro,Ndimile Kilatu, amesema kuwa, matumizi ya vyakula na viodozi vilivyoharibika vinaweza kusababisha madhara makubwa kwa watumiaji kwa kuwa kitu chochote ambacho muda wake wa matumizi umepita ni sumu.
Ndimile pia amewataka wauza vyakula wasajili vyakula vyao na TBS ili kuweza kulinda viwango vya vyakula kwa wateja wao.
Post a Comment