Header Ads

RC MALIMA AIOMBA SERIKALI KUU KUINGILIA KATI DENI LA BILIONI 20 STENDI YA MSAMVU MANISPAA YA MOROGORO

MKUU wa Mkoa wa Morogoro,Mhe. Adam Malima,ameiomba Serikali kuingilia kati deni la shilingi Bilioni 20 linaloikabili Manispaa hiyo kutokana na ujenzi wa Stendi ya Mabasi Msamvu.

Hayo ameyasema katika Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani wa  kujadili majibu ya hoja na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024 uliofanyika Juni 13-2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Manispaa ya Morogoro.

RC Malima,amesema Manispaa ilipewa Stendi hiyo na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli lakini bado mpaka sasa kuna kizungunguti juu ya deni hilo linalodaiwa na Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa (LAPF) ambao kwa sasa unajulikana kama PSSSF.

Katika hatua nyengine,RC Malima, ameipongeza Halmashauri kwa kuendelea kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato ya ndani pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo jambo lililopelekea Halmashauri kuendelea kupata hati safi.

Aidha, RC Malima,amesema Manispaa ilikuwa na hoja 16 ambapo hoja zote zilijadiliwa na baadhi ya hoja zikafungwa na nyengine zinaweza kufungwa pale CAG atakapo jiridhisha kutokana na maelekezo aliyoyatoa.

Naye, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe.Pascal Kihanga,  amemshuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuipatia Manispaa fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Manispaa ya Morogoro.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro,Emmanuel Mkongo, ameishukuru Timu ya Menejimenti ya Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro pamoja na Baraza zima la Madiwani wa Manispaa ya Morogoro  kwa kazi wanayofanya na ameahidi kuwa kutekeleza kwa wakati mapendekezo na ushauri uliotelewa Mdhibiti na  Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Ikumbukwe kwamba Ujenzi wa Stendi ya Msamvu  umekuja kufuatia Manispaa ya Morogoro kwa kushirikiana na Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa (LAPF)  kuunda  Kampuni ya ubia iliyojulikana kama Msamvu Properties Company (T) Limited ambayo ilikuwa na jukumu la kusimamia shughuli zote za stendi ikiwa ni pamoja na ukusanyaji wa ushuru wa stendi, ujenzi na uendeshaji wa miradi yote itakayokuwa inatekelezwa na Kampuni kwa niaba ya taasisi hizo mbili.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.