Header Ads

DAS WILAYA YA MOROGORO AZINDUA KAMPENI YA UTOAJI DAWA ZA MINYOO NA MATONE YA VITAMINI A KWA WATOTO (1-5) MANISPAA YA MOROGORO



KATIBU Tawala Wilaya ya Morogoro,Ruth John,amezindua huduma za Kampeni ya Utoaji dawa za Minyoo na Matone ya Vitamini A kwa watoto wenye umri wa miezi 12 yaani  miaka 1 hadi miaka 5.

Kampeni hiyo imezinduliwa Juni 10-2025 Katika Kata ya Kiwanja cha Ndege huku mamia ya wananchi wakishiriki katika uzinduzi huo.

Akizungumza na wananchi waliojitokeza katika uzinduzi huo , Ruth,amesema uzinduzi huo umeenda sambamba na Siku ya Lishe ya Mtaa (SALiKi) na ufunguzi wa Mwezi wa Afya Lishe ya Watoto (CHNM).

DAS Ruth,amesema suala la Lishe limekuwa janga kwa jamii nzima ambapo waathirika wakubwa ni Mama wajawazito na watoto chini ya miaka 5.

"Tumezindua kampeni hii lakini pia tumeona changamoto ya lishe kwa wananchi, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya imepewa jukumu kubwa katika kusimamia utekelezaji wa shughuli za lishe ,"Amesema DAS Ruth.

Aidha,amesema kwa tafiti zilizofanyika 2022 nchini, kwa mkoa wa Morogoro zinaonesha upungufu wa damu kwa wanawake walio na umri wa kuzaa (miaka 15-49) ni asilimia 47 ikiwa ni wanawake 4-5 kati ya 10,huku upungufu wa damu kwa watoto chini ya miaka 5 ni asilimia 68 ikiwa ni watoto 6-7 kati ya 10 na udumavu ni asilimia 31.

Mwisho,ametoa wito kwa wananchi kufika katika vituo vya kutolea huduma za afya kupata huduma hizo ambapo zoezi hilo limeanza rasmi Juni 10 na kumalizika juni 30-2025

Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa ya Morogoro, Dkt.Felister Stanslaus, amesema lengo la maadhimisho ya siku ya lishe ni kupata fursa ya huduma jumuishi katika eneo husika na kuweza kutambua matatizo ya kiafya  na kuyatatua.

Mratibu wa Huduma za Lishe Manispaa ya Morogoro, Ester Kawishe, amesema kuwa Kampeni ya kutoa dawa za Minyoo na Matone ya Vitamini A inahusisha  watoto wenye umri wa miezi 12 mpaka miezi 59 ( mwaka 1 - 5).

Kavishe ,amesema lengo la Mwezi wa Afya na Lishe wa watoto chini ya miaka 1-5 kila mwaka ni kutoa huduma kinga kwa ajili ya kuimarisha afya na maisha ya Mtoto.

Katika uzinduzi huo , huduma  mbalimbali zilitolewa ikiwemo  upimaji wa presha ,sukari, utoaji wa elimu ya kijinsia, elimu ya malezi na makuzi kwa watoto pamoja na elimu juu ya lishe bora kwa watoto.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.