MKURUGENZI MACHELA ATOA NENO BAADA YA MANISPAA YA MOROGORO KUIBUKA MSHINDI WA JUMLA MASHINDANO YA SHIMISEMITA
"Napenda niwapongeze sana kamati nzima kuanzia walimu waliofanya maandalizi, wadau wetu, washangiliaji na waratibu wote lakini pongezi zangu za dhati kabisa ni kwa wanamichezo wenyewe waliotuletea vikombe hivi katika mashindano haya ambayo takribani miaka 8 hayajafanyika " Amesema Machela.
Naye Afisa Michezo Manispaa ya Morogoro, Asteria Mwang'ombe,amesema kuwa ushirikiano mkubwa baina ya walimu wa michezo, juhudi za wachezaji ndiyo siri kubwa ya mafanikio kwa Manispaa kuibuka mshindi wa jumla
“Wakati wa kufanya uchaguzi wa wanamichezo tulikuwa na umakini mkubwa, tulifanya uchaguzi makini wa wanamichezo wetu, tuliwachagua kwa uwezo wao na siyo kwa upendeleo, tulicheza kwa tahadhari na kuheshimu wapinzani wetu katika michezo yetu yote, lengo likiwa ni kujenga timu imara na itakayotoa ushindani na kulinda hadhi ya Manispaa na hatimaye tukawa washindi wa jumla" Amesema Mwang'ombe.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Mashindano kwa Watumishi Manispaa ya Morogoro, Neema Gwaseko,amesema ushindi walioupata umetokana na juhudi za wanamichezo hivyo matumaini yao ushindi huo watautafsiri kwenye michuano ijayo ambapo watakuwa na kibarua cha kutetea ubingwa wao.
"Tunawashukuru wanamichezo wetu walipambana sana, na ushindi ambao tumeupata kamwe hawatabweteka na ushindi huo kwani mwakani tutaanza maandalizi mapema ili kutetea ubingwa wetu" Amesema Gwaseko.
Post a Comment