Header Ads

VIONGOZI WA DINI WAOMBWA KUTOA ELIMU KWA JAMII KUSAIDIA KUPAMBANA NA VITENDO VYA UKATILI WA KIJINSIA.




VIONGOZI wa dini Wilaya ya Morogoro  wameombwa kutoa elimu kwa jamii au waamini wao kwa ajili ya kuisaidia Serikali kupambana na Vitendo vya Ukatili wa Kijinsia wanavyofanyiwa watoto na wanawake.

Kauli hiyo imetolewa na Afisa Tarafa Manispaa ya Morogoro, Winfred Kipako,  akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Morogoro katika Mkutano wa Mafunzo ya kuhamasisha kusimamia Amani , maadili na kutokomeza ukatili wa kijinsia ulioandaliwa na Jumuiya ya Maridhiano Tanzania Wilaya ya Morogoro leo Novemba 2/ 2022 katika Ukumbi wa Kilakala Soko Kuu la Chifu Kingalu.

Akizungumza katika mkutano huo, Kipako,  amesema viongozi hao wana mchango mkubwa wa kuibadilisha jamii kuachana na vitendo hivyo kwani kuwapeleka jela wahalifu haisaidii kwa kiasi kubwa kupunguza tatizo hilo.

" Elimu ni muhimu viongozi wa dini wanaweza kusaidia kupambana na vitendo hivi kuwafunga wahalifu peke yake haisaidii kwani wakiwa jela watafanya tena lakini wakijengwa kiimani itasaidia matendo haya kupungua," Amesema Kipako.

Katika hatua nyengine, Kipako, amewaomba Wenyeviti wa Mitaa kuwabaini wakazi na wahamiaji wapya wenye tabia mbaya kabla hawajaleta madhara kwa watoto hivyo kupunguza vitendo hivyo.

Hata hivyo, amewasahauri wazazi na walezi kuacha kuwashirikisha watoto ugomvi wao na kuwakumbusha kutenga muda wa kuzungumza na watoto ili iwe rahisi kupewa taarifa endapo wanafanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Amewataka wazazi kuacha tabia ya kuwatuma watoto muda wa usiku ili kuwaepusha na watu wanaoweza kuwafanyia vitendo vya ukatili huo.

Mwisho amewataka wenyeviti kuacha tabia ya kujihusisha na mauziano ya ardhi pamoja na kuwataka wananchi kujenga kwa kufauata utaratibu wa kuwa na vibali vya ujenzi.

Naye, Afisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Morogoro, Joyce Mugambi,  amewakumbusha wazazi kutenga muda wa kuzungumza na watoto wao mambo mbalimbali ikiwemo kuwahoji endapo wamefanyiwa ukatili wa kijinsia. 

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mariadhiano Mkoa wa Morogoro, Juma Ngodavi, amesema mmomonyoko wa maadili umekuwa mkubwa hivyo kuna haja sasa wazazi wakawa karibu na watoto na kuwapa elimu ya kiroho  ili kuepukana na ukatili wa kijinsia.

Aidha, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhaino Wilaya ya Morogoro, Azizi Viguro, amewaomba viongozi wa dini wenzake kujikita katika kutoa elimu ya kiroho na mafundisho ya kiimani katika maeneo yaliyoshamiri vitendo vya ukatili wa jinsia.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.