MANISPAA YA MOROGORO YAPONGEZWA UTEKELEZAJI UGAWAJI DAWA ZA KICHOCHO NA MINYOO YA TUMBO.
AFISA Mpango kitengo cha kichocho na Minyoo ya tumbo Wizara ya afya Mpango wa kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele,Mohamed Nyati, amesema kuwa ameridhika na maandalizi ya watoto shuleni kwani kila shule imewandaa watoto vizuri kwa kuwa elimisha umuhimu wa kumeza dawa za minyoo ya tumbo na kichocho.
Kauli hiyo ameitoa leo Novemba 15/2022 akiwa katika ziara ya kuzitembelea shule zilizopo Manispaa ya Morogoro kwa ajili ya kuangalia mwenendo mzima wa zoezi la ugawaji dawa za minyoo ya kichocho na minyoo ya tumbo kwa wanafunzi wa Shule za Msingi za Serikali na binafsi.
Nyati,amesema kuwa utekelezaji wa zoezi hilo unaendelea vizuri kwani kila shule imeandaa mazingira safi ya kugawia dawa na pia walimu wamehakikisha kila mtoto ana pata chakula cha kutosha kabla ya kunywa dawa hizo.
Naye Mratibu wa Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele Manispaa ya Morogoro, Dr.Warialanga Nnko,amewashukuru Waalimu na Wazazi kwa ushirikiano wao katika kufanikisha zoezi hilo.
"Nimeridhishwa na zoezi la ugawaji wa dawa, mpaka sasa hakuna madhara yoyote na changamoto yoyote ambayo imejitokeza, kikubwa niwaombe waalimu wazidi kutoa elimu kwa wazazi ili kufanikisha zoezi hilo" Amesema Nnko.
Mwisho, Nnko, amewasisitiza Walimu hao kuendelea kuwa karibu na wanafunzi hao pamoja na kuwapatia elimu ya kuwaondoa hofu baada ya kunywa dawa hizo.
Utekelezaji wa zoezi la ugawaji wa dawa za minyoo ya tumbo na minyoo ya kichocho kwa wanafunzi wenye umri wa miaka 5-14 kwa Shule za Msingi Manispaa ya Morogoro umeanza leo Novemba 15/2022 na linatarajia kukamilika Novemba 16/2022 ambapo zoezi hilo linatekelezwa chini ya usimamizi wa walimu wakuu na walimu wa afya kwa kila shule husika.
Miongoni mwa baadhi ya shule zilizotembelewa ni Shule ya Msingi Mkundi, Mgulu wa ndege, Ahmadya, Carmel, Mwenge pamoja na Bensal.
Post a Comment