MANISPAA YA MOROGORO YAFUNGUA MAFUNZO YA KINGA TIBA YA DAWA YA KICHOCHO KWA WAALIMU WAKUU SHULE ZA MSINGI NA WAALIMU WA AFYA.
HALMASHAURI ya Manispaa ya Morogoro imefungua mafunzo kwa waalimu wakuu wa shule za Msingi ikiwamo na shule binafsi , waalimu wa afya kwa ajili ya kuwaandaa katika kusimamia zoezi la ugawaji wa dawa za kichocho kwa wanafunzi wenye umri wa miaka 5-14 linalotarajia kufanyika tarehe 15/11/2022.
Akizungumza katika ufunguzi huo, Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa ya Morogoro, Bertha Mahanga, amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha zoezi hili la ugawaji wa dawa linatekelezwa vizuri ili kila mtoto/mwanafunzi aweze kupewa dawa hizo.
Mahanga, amesema Manispaa imejipanga vizuri na imeweka malengo mkakati ya utekelezaji wa mpango wa kugawa dawa Shuleni ikiwamo upatikanaji wa huduma hiyo katika vituo vya huduma ya afya pamoja na kujenga uwezo wa utekelezaji wa mpango huo kwa jamii ili jamii iwe na afya bora.
" kichocho husababishwa na minyoo inyoitwa jamii ya Schistosoma ambao unaenezwa na konokono kwa kutoa vimelea kupitia maji yaliyotuama, lakini athari yake husababisha damu kutoka kwenye njia ya mkojo na choo, na baadae inaweza kusababisha saratani ya tumbo, kibofu cha mkojo na ini" Amesema Mahanga.
Naye Mratibu wa Magonjwa yasiyopewa kipaumbele Manispaa ya Morogoro, Dr.Warialanga Nnko,amesema kuwa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ni magonjwa ambayo yamo ndani ya jamii zetu, hivyo kwa mpango huu wa ugawaji wa dawa hizi utaleta matokeo chanya na kuwakinga watoto na kichocho.
" Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ni magonjwa ambayo yamo ndani ya jamii ni usubi, Matende na mabusha, Trakoma, kichocho na minyoo ya tumbo, hivyo katika kuona kasi ya maambukizi ya ugonjwa wa kichocho inapungua , Serikali ikaona kuja na mpango wa dawa kwa watoto miaka 4-15 kwani wao wapo katika uhatari wa kupata ugonjwa huo kwa haraka kutokana na kuogelea katika madimbwi ya maji " Amesema Nnko.
Mmoja wa watoa mafunzo , Dr. Caroline Sakaya, amezitaja njia za kujikinga na magonjwa ikiwamo kutumia dawa za kutibu na kudhibiti magonjwa haya ambazo hutolewa kila mwaka kwa jamii iliyoathirika, kuzingatia usafi wa uso na mwili, usafi wa mazingira, kutokuoga kwenye maji yasiyo safi na yaliyotuama (bwawa), kujikinga kuumwa na inzi au mbu, na kutoa elimu ya afya ya jamii.
Katika mafunzo hayo waalimu walipewa majukumu ikiwamo kutoa elimu ya afya kuhusu manufaa na maelekezo ya umezaji dawa husika kwa kiongozi wa shule, wazazi, na wanafunzi, kuandikishwa walengwa (wanafunzi) kwenye rejista, kuaandaa chakula kwa ajili ya wanafunzi kabla ya kumeza dawa na Dawa hiyo imezwe ndani ya masaa mawili baada ya kula chakula.
Post a Comment