WANAWAKE WAJANE WATAKIWA KUJIWEKEA MALENGO 2022.
Wakati tunaelekea kuumaliza mwaka 2021
na kuanza mwaka 2022, Wito umetolewa kwa Wanawake wajane na wale wanaoishi na watoto bila wenza wao kujiwekea
malengo na mikakati mathubuti ya kufanya shughuli za uzalishaji mali ili waweze
kumudu gharama za maisha na malezi ya watoto.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa asasi isiyo ya Kiserikali ya UECO, Sophia Kalinga,ambaye pia ni mjane, wakati wa kongamano la wanawake wajane wa Manispaa ya Morogoro lililofanyika Desemba 28/2021 katika Ukumbi wa Kilakala Soko Kuu la Chifu Kingalu.
Akizungumza katika
kongamano hilo, Kalinga amesema kuwa ujane sio laana hivyo wanawake wajane
wasijione kuwa hawawezi kusimama peke yao, bali wanatakiwa kujithatiti katika
kufanya shughuli mbali mbali za uzalishaji mali ili waweze kumudu kulea familia
walizoachiwa na waume zao.
“Achane kuhuzunika, tumieni
fursa za mikopo kutoka kwenye taasisi za kifedha, undeni vikundi vya
ujasiriamali, Halmashauri zetu zina fungu maalumu la mikopo ya ujasiriamali kwa
ajili ya akina mama, vijana na watu wenye ulemavu, msiogope, mwende mkakope,
jambo la msingi ni kujiwekea malengo na kujidhatiti kikamilifu katika kufanya
kazi kwa bidii.” Alisema Sophia.
Sophia aliwataka wanawake wajane na wale ambao wanalea watoto pasipo baba ‘Single Mothers’ kujiepusha na mahusiano ya mapenzi holela kwani kufanya hivyo hakutawapa unafuu wa maisha bali wanaweza kuambukizwa magonjwa ya ngono ikiwa ni pamoja na UKIMWI, yatakayopelekea kuwaacha watoto wao yatima.
Kongamano hilo liliuhudhuriwa na zaidi ya wanawake 400.
Post a Comment