WANANCHI WA KIVAZA, MFINE NA MLULU KATA YA LUHUNGO WALIA NA VIVUKO VYA MADARAJA.
WANANCHI wa Mitaa ya Kivaza, Mfine na Mlulu Kata ya Luhungo Manispaa ya Morogoro , wameiomba Serikali kuwasaidia ujenzi wa Vivuko vya madaraja vinavyounganisha Mitaa 3 ikiwamo Mtaa wa Kivaza, Mfine na Mlulu.
Wakizungumza kwa nyakati tofautitofauti katika Mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kutatua kero za Wananchi wa Mitaa hiyo uliandaliwa na Mtendaji wa Kata ya Luhungo John Joseph ikiwa ni ziara zake za kuwasikilza Wananchi katika Mitaa yake.
Kutokana na adhaa hiyo wananchi hao wameiomba Serikali kuwajengea madaraja kwenye maeneo hayo yanayounganisha Mitaa yao ili kuwaweze wananchi na vyombo vya moto kupita kwa urahisi zaidi muda wote tofauti na ilivyo kwa hivi sasa ambapo wanapita kwa shida kubwa wakati na kushindwa kuvuka kabisa kipindi cha Mvua zinaponyesha.
Regina Pius Dilunga, akizungumza kwa niaba ya wakazi waliohudhuria kwenye Mkutano huo,ameiomba serikali kuangalia kwa jicho la upana kwenye maeneo ya vivuko hivyo kutokana na shida kubwa wanayokabiriana nayo haswa katika kipindi cha mvua.
"Maji yakijaa kwenye maeneo haya ya vivuko hakuna gari lolote wala Mtutu yeyote anayeweza kupita , hali hii kuna hatari siku nyingine akina mama wajauzito wanaweza kujifungulia hapa na wakakosa msaada kutoka kwa wahudumu wa afya, lakini pia watoto wetu mvua zikinyesha hawaendi shule, shughuli za maendeleo zina simama, tunaiomba Serikali ituangalie kwa jicho la tatu sisi tuliopo huku pembezoni mwa mji" Amesema Regina.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa serikali ya Mtaa wa Mlulu, Saidi Kondo,akizungumza kwa niaba ya Wenyeviti wenzake, amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo kwenye maeneo hayo ya madaraja yanayounganisha Mitaa 3, huku akisema bado wananchi wanateseka kutokana na kukosa huduma ya vivuko kwa muda wa miaka mingi.
"Hivi karibuni nimempoteza Mke wangu aliyesombwa na Maji katika vivuko hivi, suala la Vivuko kwetu limekuwa ni changamoto sugu , hili tatizo ni tatizo la muda mrefu lisilopatiwa ufumbuzi, haya maeneo ambayo hayana vivuko ni mkondo wa maji yanayotoka milimani,hivyo kuna kila sababu kwa serikali kutumia jitihada zake za kujenga Vivuko ili Wananchi waweze kupitika kwa msimu wote" Amesema Kondo.
Mwisho, Wananchi hao wamesema hawatashiriki kuchangia shughuli zozote za Maendeleo mpaka suala lao la Vivuko kukamilika.
Naye Mtendaji wa Kata ya Luhungo, John Joseph , amewashukuru wananchi hao kwa kushiriki kikamilifu katika Mkutano wake ambapo katika Mkutano huo ameweza kuzungumza mambo na hatua mbalimbali ambazo zinafnaywa Uongozi wa Manispaa ya Morogoro kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya katika kuhakikisha changamoto hiyo ya ukosefu wa Vivuko inatatuliwa.
"Hii ni ziara yangu ya kikazi ya kupita katika Mitaa yangu yote kusikiliza na kutatua kero za Wananchi, kero kubwa zaidi hapa Luhungo hususani katika Mitaa hii mitatu iliyotajwa ni ukosefu wa Vivuko, nimewaomba Wananchi kuwa wavumilivu kwani Seriali yao ni sikivu na ipo tayari kuhakikisha tatizo hil linatatuliwa na wananchi kuendelea na shughuli zao za maendeleo bila vikwazo" Amesema John.
Amesema ziara hiyo itaendelea katika mitaa iliyobakia ya kusikiliza na kutatua kero za Wananchi.
Miongoni mwa Vivuko ambavyo vinatakiwa kujengwa ni pamoja na kivuko cha Mto Mzinga, Kivuko cha Mto Maunga na Kivuko cha Mto Mlulu.
Post a Comment