KAMATI YA FEDHA MANISPAA YA MOROGORO YAPONGEZA KASI YA UJENZI WA ZAHANATI UNAOENDELEA.
KAMATI ya Fedha Manispaa ya Morogoro imepongeza kasi ya ujenzi wa Zahanati unaofanywa na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ambapo mpaka sasa Halmashauri ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha Zahanati 5 kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo.
Pongezi hiyo imetolewa leo mara baada ya kumalizika kwa ziara ya Kamati ya Fedha ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo ikiwamo ujenzi wa Madarasa mapya yanayojengwa kupitia mpango wa UVICO-19.
Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Fedha, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro na Diwani wa Kata ya Mazimbu , Mhe. Pascal Kihanga, amesema kuwa Manispaa ya Morogoro kitendo cha kukamilisha Zahanati hizo kutapelekea kusogeza karibu huduma za afya kwa Jamii.
“Uongozi unaweza kufanya mabadiliko makubwa sana. Menejimenti mnaongea lugha moja hicho ni kitu kizuri sana na ndio maana kwa pamoja mnaweza kutekeleza haya yote, niwapongeze Manispaa kwa kushirikiana na Madiwani kwa maono yenu, ni muda mrefu sasa Manispaa haijawahi kukamilisha miradi ya namna hii nawapongeza sana timu ya Menejimenti mkiongozwa na Mkurugenzi wa Manispaa kipindi cha miaka 5 iliyopita na leo tulivyoona nimeona kuna mabadiliko makubwa sana niwapongeze sana" Amesema Kihanga.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Ally Machela, amesema kuwa Manispaa imejiwekea utaratibu wa kufanya vikao viwili kila wiki ambapo menejimenti hujadili taarifa za mapato katika vyanzo vyote zikiwemo hospitali vituo vya afya na Zahanati jambo ambalo Wakuu wa Idara hushiriki na kutoa mawazo juu ya jitihada za ukusanyaji mapato.
“Kwenye makusanyo huwa tunakusanya kwa asilimia kubwa, hii imepelekea Manispaa kuweza kupeleka fedha katika miradi ya afya na ndio maana kwa sasa tupo katika kukamilisha Zahanti 5 kabla ya kumaliza mwaka huu wa 2021 , Manispaa kupitia mapato ya ndani tutaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kadri tunavyozidi kupata makusanyo na kutenga fedha zitakazo sukuma miradi kwa ajili ya kuwahudumia Wananchi" Amesema Machela.
Aidha, Diwani wa Kata ya Mwembesongo ambaye ni Mjumbe wa Kamati hiyo, ameshauri kuwa ni vyema katika Zahanati hizo mara baada ya kukamilika kuweka uhifadhi wa mazingira kwa kupanda miti ya matunda kwenye bustani zinazozunguka maeneo ya Zahanati hizo.
Post a Comment