Header Ads

'MARUKU UJENZI BILA KIBALI' RC SHIGELA.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Martine Shigela, akizungumza na wananchi wa Kata ya Lukobe.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Albert Msando akizungumza na wananchi wa Kata ya Lukobe.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Martine Shigela (kushoto), Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro Mhe. Pascal Kihanga (katikati) , Diwani wa Kata ya Lukobe , Mhe. Selestine Mbilinyi (kulia) wakiteta jambo katika Mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero za Wananchi Kata ya Lukobe.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Ally Machela, (aliyevaa Suti nyeusi) akifuatilia kwa umakini Mkutano wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi wa Kata ya Lukobe, ulioitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Martine Shigela.

MKUU wa Mkoa wa  Morogoro, ametoa onyo kwa Mwananchi yeyote wa Mkoa wa  Morogoro kuanzisha ujenzi bila ya kuwa na kibali cha ujenzi.

Onyo hilo amelitoa Novemba 05/2021 , katika Mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kutatua kero za Wananchi Kata ya Lukobe Manispaa ya Morogoro.

 Akizungumza na Wananchi wa Kata ya Lukobe waliojitokeza katika Mkutano huo wa hadhara, RC Shigela, amesema lazima wananchi  wazingatie sheria zilizokubalika katika kusimamia jambo fulani kwani kwenda kinyume na sheria ni sawa umeidharau Serikali yako na wale walioitunga sheria hiyo.

RC Shigela , amesema kuwa Serikali haina mpango wa kubomoa nyumba za wananchi isipokuwa wanatakiwa kujenga kwa kufuata utaratibu ikiwa ni pamoja na kupata kibali cha ujenzi.

"Mtu  yeyote anayejenga mjini au  mahali popote bila kufuata utaratibu wa kumilikishwa yaani kiwanja ambacho hakijapimwa, hajamilikishwa, hana kibali cha wenye mamlaka ya mji unaohusika ujue anajipeleka kwenye hatari ya kuvunjiwa na kuondolewa jengo lake. nitoe angalizo lazima tuzingatie sheria za Mipango miji ili tuepukane na migogoro hii ya kuonekana wavamizi na kuingia hasara zisizo za kilazima" Amesema RC Shigela.

"Ni  marufuku kuwabariki watu waliojenga kwa kuvunja sheria bila vibali,serikali yetu imedhamiria kupunguza na  kuondoa migogoro  kwa  wananchi waliojenga kiholela na kupima maeneo yote ambayo hayajapimwa, kwahiyo Sheria haijasema pembezoni mwa mji watu wajenge tu, sasa usiendelee kujenga na kama umejenga anza sasa kumwambia  fundi wako aache kujenga na ujenzi hadi upate kibali.” Ameongeza RC Shigela.

Mwisho, amewaagiza Maafisa ardhi wa Halmashauri zote kuhakikisha wanatumia njia nzuri ya maelewano na wahusika wanaowakuta katika maeneo yenye mgogoro  wahakikishe kabla ya kuwaondoa  wanakaa chini na kuangalia utaratibu mzuri wa kuwaondoa kwa makubaliano ya pande zote mbili na sio kutumia nguvu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Albert Msando, amesema kwa kutambua uwepo wa migogoro ya ardhi katika Wilaya hiyo , amejipanga kikamilifu kuhakikisha migogoro hiyo inakwisha au inapungua kwa kiasi kikubwa  ili kila mtu ambaye amenyimwa haki ya ardhi apate haki yake kutokana na utaratibu uliopo.

DC Msando, amesema asili ya migogoro ya ardhi inatokana hasa na mgongano wa uhalali wa umiliki pamoja na uvamizi wa maeneo ya wazi yaliyotengwa kwa shughuli za jamii ambazo sababu hizo ni changamoto za muda mrefu na juhudi zinafanyika kuzipatia ufumbuzi.

"Tunataka kuhakikisha migogoro hii inakwisha katika Wilaya yetu ya Morogoro, ili kupata ufumbuzi usio na shaka , tayari tushaunda kamati ndogo itakayohusika katika kushughulikia matatizo  na changamoto za ardhi  ili kufupisha mlolongo unaowapotezea muda walioko kwenye migogoro na kuhakikisha mwenye haki anapewa haki yake bila kuyumbishwa ,

Kwa upande wa  Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro , Mhe. Pascal Kihanga, amewataka wale wote wenye changamoto ya migogoro ya ardhi  ili waweze kupata haki zao , na zoezi la utoaji haki zao liende kwa ufanisi amewaomba wananchi kufuata utaratibu wa kuanzia kupita katika ngazi za Watendaji wa chini kabla ya kufikisha ngazi za juu na kila muhusika ahakikishe anakuwa na vielelezo vyote halali vinavyoweza kutumika katika kufikia uamuzi.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro , Ally Machela, amesema atahakikisha migogoro yote inayoendelea katika Kata na maeneo yote ya Manispaa ya Morogoro inatatuliwa kwa njia ya ushirikishwaji.






No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.