Header Ads

RAS MOROGORO AFUNGA MAFUNZO YA PEPMIS, ATAKA UWAJIBIKAJI NA UAMINIFU


KATIBU Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Alhaji Dkt. Mussa Ali Mussa, amewataka watumishi wa umma mkoani humo kuwajibika na kuwa waaminifu katika kujaza mfumo wa mwongozo wa utekelezaji wa usimamizi wa utendaji kazi (PEPMIS), ili kuhakikisha mkoa huo unatekeleza kikamilifu agizo la Serikali.

Dkt. Mussa alitoa kauli hiyo tarehe 28 Juni 2025, wakati akifunga mafunzo ya siku sita kuhusu ujazaji wa mfumo huo wa PEPMIS, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, ikiwa ni siku ya mwisho ya mafunzo hayo mkoani humo.

Amesema kuwa wakuu wa seksheni, idara na vitengo wasipokuwa waaminifu na kuruhusu ujazaji holela wa taarifa katika mfumo huo, itakuwa vigumu kufikia malengo ya Serikali.

Aliongeza kuwa viongozi hao watakuwa wameshiriki moja kwa moja katika kuushusha mkoa huo kiutendaji, ambao kwa sasa uko nafasi ya pili kitaifa kwa ujazaji wa mfumo wa PEPMIS, na kwa upande wa vyuo, Mkoa wa Morogoro ndio kinara.

“Ombi langu sasa, kila mmoja atimize wajibu wake anavyotakiwa… tujaze fomu hizo kwa mantiki kwamba kila mmoja anajaziwa kwa kile anachostahili,” alisisitiza Dkt. Mussa.

Mafunzo hayo ya PEPMIS yalianza tarehe 23 Juni 2025, yakitolewa na maofisa kutoka Ofisi ya Rais – Utumishi, yakiwahusisha makundi mbalimbali ya watumishi wa umma, hususan wakuu wa idara na vitengo kutoka halmashauri za mkoa huo, Sekretarieti ya Mkoa, na taasisi za umma zilizoko mkoani humo.

Mfumo wa utendaji kazi, yaani Performance Management Information System (PEPMIS), una lengo la kuongeza ufanisi na uwajibikaji kwa watumishi wa umma. 

Pia ni mfumo huo  nyenzo muhimu ya kiutumishi inayosaidia mtumishi wa umma kuweka malengo yake ya utendaji kazi na kuyatekeleza ipasavyo.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.